Advertisement

Advertisement

.

.

Mixer

Mixer

Saturday, 17 March 2018

Jafo ataka maofisa habari watengewe fedha


Selemani Jafo

WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Selemani Jafo ametoa agizo kwa ofisi za mikoa na halmashauri zote nchini kutenga fedha kwa ajili ya ununuzi wa vifaa kwa vitengo vya mawasiliano ili viweze kutekeleza majukumu yake. 

Jafo ametoa agizo hilo jijini Arusha alipokuwa akifunga Kikao Kazi cha 14 cha maofisa mawasiliano serikalini uliohudhuriwa na maofisa mawasiliano 300 kutoka katika taasisi, idara na wakala wa serikali, mikoa, majiji, iji na halmashauri zote nchini. 

“Kuanzia mwaka ujao wa bajeti, makatibu tawala wa mikoa na akurugenzi wa halmashauri, majiji, manispaa na miji waweke kipaumbele kwa kutenga fedha za kununua vifaa muhimu kwa ajili ya maofisa habari na mawasiliano ili waweze kutekeleza majukumu yao ipasavyo,” amesema Jafo.
Vile vile ameagiza maofisa habari wapewe ushirikiano wa kutosha na wakuu wa idara kwa kuwapa taarifa na takwimu za idara zao ili kuwawezesha maofisa hao kutoa taarifa muhimu za Serikali kwa vyombo vya habari na wananchi kwa wakati na bila vikwazo.
Aidha, amewataka viongozi wa mamlaka ya serikali za mitaa kutambuua kuwa ofisa habari ndiye mtendaji mkuu katika masuala ya uandaaji wa habari, hivyo ni muhimu maofisa hao kuingia katika vikao mbalimbali ili wapate uelewa wa masuala mbalimbali ya kimaamuzi yanayofanywa na uongozi.
Kwa upande wake, katibu mkuu wa Wizara ya Habari Utamaduni Sanaa na Michezo, Susan Mlawi amesema mada mbalimbali zimetolewa kwa lengo la kuwajengea uwezo maafisa hao, ambapo miongoni mwa mada hizo ni pamoja na umuhimu wa mawasiliano ya kimkakati katika kuisemea Serikali na tathmini ya utendaji katika mwaka 2017, maadili ya usalama katika kazi ya kuitangaza na kuisemea serikali pamoja na wajibu wa maofisa habari katika mkakati wa kitaifa wa kupambana na maafa.
Mkuu wa mkoa wa Arusha, Mrisho Gambo amesema ofisi yake itashirikiana na Wizara ya Habari Utamaduni Sanaa na Michezo kuhakikisha maazimio yote yaliyoafikiwa katika mkutano huo yanatekelezwa katika vitengo vyote vya mawasiliano vya halmashauri zote za Mkoa wa Arusha.
Mkutano wa maofisa mawasiliano serikalini unafanyika kila mwaka, ambapo kwa mwaka huu unafanyika kwa mara ya 14.  Mkutano huo umeandaliwa na Wizara ya Habari Utamaduni Sanaa na Michezo kwa kushirikiana na chama cha maofisa mawasiliano.
Maofisa habari

Aliyekutwa na mihuri ya baraza la mitihani mikononi mwa polisiJESHI la polisi linamshikiria Selemani Masoud (68), mkazi wa Yombo Kilakala Dar es Salaam kwa tuhuma za kukutwa na nyaraka mbalimbali za serikali ikiwemo kughushi mihuri na vyeti feki vya vyuo.
Akizungumza na waandishi wa habari, Kamanda Mambosasa amesema Machi 13, mwaka huu jeshi hilo lilipata taarifa za Kiitelijensia kuwa kuna kundi la watu linalojihusisha kutengeneza vyeti feki, mihuri na nyaraka mbalimbali za serikali katika eneo hilo.
Makachero wa kikosi kazi cha polisi walifika eneo la nyumba ya mshukiwa na kuanza upekuzi kwa kushirikiana na uongozi wa serikali ya mtaa kufanikisha kumkamata mtuhumiwa na nyaraka hizo.
Mtuhumiwa alikutwa na mihuri 53, ukiwemo wa Baraza la Mitihani Tanzania (NECTA), wa Chuo cha Ufundi Stadi (Veta), Chuo Kikuu cha Dar es Salaam UDSM, Chuo Kikuu cha Sokoine (Sua), Chuo cha Bandari, Chuo Kikuu Huria cha Tanzania (OUT), Mtwara University, Muhuri wa Mamlaka ya Mapato Tanzania(TRA), Muhuri wa cancelor wa UDSM, Chuo cha Usafirishaji (NIT),Chuo cha usimamizi wa Fedha (IFM), Bodi ya uhasibu (NBAA), Chuo cha Tumaini(TUDARCO), Chuo cha Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere, Rita, Health Laboratory, JKT Makao makuu na Marine Association of certified.
Mwingine wa ni wa mahakama ya hakimu mkazi Kisutu Dar es Salaam, Chuo cha uhasibu Arusha, Chuo cha utumishi wa umma, wa Wizara ya Maliasili na utalii, Mkurugenzi wa Jiji Eastern London, Mkuu wa shule Marangu, Mkuu wa shule ya Songambele, Mbagala Nursing, Msajili wa Ndoa, Shule ya Magereza, Medical Board of Tanganyika, Mkuu wa shule Kaselya Sec, Glory of Nursing, Director of Tanzania public service, Shule ya Sekondari Kibasila, ofisa elimu mkoa wa Kilimanjaro, Mwalimu mkuu shule ya Msingi Mgulani na mkuu wa shule ya sekondar Kyaka.
Jeshi la polisi linaendelea na upelelezi ili kubaini mtandao mzima anaoshirikiana nao ili kuhakikisha linawatia mbaroni wote hata kama ni watumishi wa umma.Watumia jina la Rais Kikwete kujipatia fedha kwa udanganyifu


 Rais Jakaya Kikwete

JESHI la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, linawashikilia wanawake watatu kwa kosa la kutumia jina la Rais mstaafu, Jakaya Kikwete na familia yake kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu.
Akizungumza na waandishi wa habari jana Dar es salaam, Kamanda wa Polisi wa kanda hiyo, Lazaro Mambosasa amesema Februari 23 mwaka huu kuliripotiwa kuwepo watu wanaotumia jina la kiongozi huyo kushawishi wengine kupata mkopo wa fedha kwa kujitangaza kupitia ukurasa wa facebook uitwao, ‘Jakaya Kikwete Focus Vicoba’ na ‘Ridhiwan Kikwete Focus Vicoba’
Kamanda Mambosasa amewataja washukiwa hao kuwa ni Mase Uledi (41), mkazi wa Kitunda, Khadija Khamis (42), mkazi wa Tabata na Mwange Uled (33), mkazi wa mkoa wa Bukoba.
Washukiwa hao walikamatwa wakiwa na simu za mkononi 12 zenye laini za mitandao mbalimbali huku wakiwa na nyingine 10 zisizo kuwa ndani ya simu ambazo huzitumia ili kufanikisha uhalifu huo.
Washukiwa hao walifungua ukurasa huo wa facebook na wamekuwa wakitumia laini hizo za simu kuwapigia na kuwatumia ujumbe mfupi wananchi ili kuwashawishi kujiunga kwenye taasisi hizo na kufanyia miamala ya fedha kutoka kwa wakopaji wanaoshawishika.
Aidha, Kamanda Mambosasa amesema watuhumiwa hao watafikishwa mahakamani kujibu tuhuma zinazo wakabili.
Lazaro Mambosasa

Miaka miwili ya Makonda Dar awaomba msamaha wananchi wakePaul Makonda
MKUU wa mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda amewaomba msamaha wananchi wa mkoa huo  ambao ameshindwa kutimiza ndoto ya kuwafikia na kusema ana amini ataendelea kuwatumikia na kujitahidi kugusa maisha ya kila mmoja.

Makonda amesema hayo jana iikiwa ni siku mbili baada ya kutimiza miaka miwili tangu ateuliwe kuwa mkuu wa mkoa wa Dar es Salaam na kusema kuwa ndani ya miaka hiyo ana amini amegusa maisha ya watu kwa kutumia kipaji chake na uwezo wake wote wa uongozi.

"Asante Mungu kwa neema zako, kama usingekuwa upande wangu na Dunia iseme sasa. Nawashukuru sana watumishi wenzangu kwa kunivumilia na kunielewa katika kutimiza majukumu yangu.

“Zaidi nawashukuru wananchi na nina imani nimejitahidi kuwatumikia kwa moyo wangu wote na vipaji vyote na pale niliposhindwa kutimiza ndoto yenu mnisamehe," amesema.

Makonda amewaahidi wakazi wa mkoa wake kuwa ataendelea kujituma zaidi ili ayaguse maisha ya kila mmoja wao.

“Kwakutambua mchango wenu ninaandaa siku ya kuwatambua na kuwatunuku tuzo kama asante yangu kwenu,” amesema.

Zuma akabiliwa na mashtaka ya rushwa


Jacob Zuma

ALIYEKUWA rais wa Afrika Kusini, Jacob Zuma amepatikana na mashtaka 16 ya rushwa inayohusishwa na mamilioni ya dola yaliotumika katika mpango wa silaha.
Mashtaka hayo ambayo Zuma amekataa kuhusika yanajumuisha udanganyifu aliofanya ili kujipatia fedha na utakatishaji wa fedha.
Zuma mwenye umri wa miaka 75,chama chake cha ANC kilimlazimishaa kuachia madaraka yake mwezi uliopita. Zuma alipigiwa kura ya kutoaminiwa mara ya tisa katika bunge kabla hajaachia ngazi.
Mwendesha mashtaka mkuu Shaun Abraham amesema ana amini kuwa kuna sababu ya kuwa na mtazamo chanya kuhusu hukumu ya kesi hii.
Msambazaji wa silaha kutoka Ufaransa Thales yeye pia atakabaliwa na mashtaka. .Taarifa kutoka AFP zinasema Thales amekataa kuongea chochote kuhusu suala hilo.
 Zuma anatuhumiwa kutaka rushwa kutoka kwa Thales kwa nia ya kuboresha maisha yake ya kifahari.mshauri wake wa fedha wakati huo alikutwa na hatia ya kuomba rushwa hizo mwaka 2005 na Zuma alimfukuza kazi yake ya usaidizi wa rais.
Mashtaka ya awali dhidi ya Zuma yalikuwa yameondolewa muda mfupi kabla ya kuwa rais mwaka 2009.
Kwa sasa anakabiliana na shitaka moja la kusababisha ghasia,mashtaka mawili ya rushwa,shtaka moja la rushwa na mashtaka 12 ya udanganyifu.

Wajua kabichi inasaidia kuondoa tatizo la kutoka maziwa kupita kiasi?

Kabichi


BAADHI ya kinamama wanaonyonyesha wamekuwa wakikabiliwa na hali ya kutokwa maziwa mengi, hivyo kuwa kero kwao na watoto wao.

Mama mwenye tatizo hilo atumie majani ya kabichi, maua ya yasmini na njegere kuondokana nalo.

Kabichi

Ponda majani ya kabichi, paka kwenye maziwa ya mama ili kuyafanya yawe laini kuzuia utaaji maziwa ikiwa ni mengi kupita kiasi.

Maua ya yasmini

Bandika kwenye maziwa ya mama maua ya yasmini yaliyopondwa yanasaidia kupunguza utoaji wa maziwa na kuvimba.

Njegere

Pasha moto mbegu na majani ya njegere vilivyopondwa pamoja, paka kwenye maziwa ya mama. Tiba hii inasaidia kupunguza utoaji maziwa kwa wingi na kulainisha maziwa ya mama.

Mchanganuo huu umeletwa kwako na Mtaalamu wa tiba, lishe na virutubisho, Abdallah Mandai.

Kwa anayesumbuliwa na tatizo lolote la kiafya karibu makao yetu makuu, Ukonga Mongolandege, Dar es Salaam au wasiliana na Mtaalam Mandai kwa ushauri au kujipatia kirutubisho, anapatikana kwa simu +255745900600 au barua pepe dkmandaitz@gmail.com.

Vigogo wakutana kutafuta mbinu za kumaliza mgogoro wa ardhi Kia


Vig

Vigogo waliokutana kujadili mgogoro wa ardhi Kia wakiangalia ramani ya wanavijiji.


WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Rais (Tamisemi), Selemani Jafo amekutana na mawaziri wa Ujenzi na Ardhi kutafuta suluhu ya mgogoro wa ardhi baina ya wananchi na mwendeshaji wa Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro (Kia), Kampuni ya Kadco.

Jafo amekutana jana na Waziri wa Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi, Profesa Makame Mbarawa na Naibu Waziri wa Ardhi, Angelina Mabula kujadili mustakabali wa mgogoro huo uliodumu karibu miongo mwili.

Mgogoro huo unahusisha zaidi ya kaya 1,200 zilizopo katika mikoa ya Kilimanjaro na Arusha zinazotakiwa kupisha upanuzi wa uwanja huo.

Kaya hizo zipo katika vijiji vilivyopimwa kisheria lakini maeneo ya vijiji hivyo yanaingiliana na eneo la uwanja  wa Kia na hivyo kusabisha mgogoro baina ya menejimentinti ya uwanja huo na wananchi hao.

Hali hiyo ilipelekea kuundwa timu ya ufuatiliaji na utafutaji wa suluhu ya mgogoro huo ambayo inaundwa na wizara tatu za Tamisemi, Ujenzi na ya Ardhi wakuu wa mikoa ya Kilimanjaro na Arusha na wataalamu kutoka katika sekta mbalimbali za ardhi na mawasiliano ya anga.

Kikao hicho kilimalizika kwa kuazimia kuwa vijiji hivyo vifanyiwe uthamini upya ili wananchi wa maeneo hayo walipwe fidia ili kuacha maeneo hayo kwa ajili ya upanuzi wa kiwanja cha ndege.

Kwa pamoja viongozi hao wamekubaliana kuanza mchakato wa kufuta hati za vijiji hivyo na kuanza mchakato wa kuwaelimisha wananchi kuhusu  umuhimu wa eneo hilo kwa maslahi mapana ya taifa.

Mgogoro kati ya wananchi wanaozunguka uwanja wa ndege wa Kia na kampuni ya Kadco umekuwepo tangu mwaka 1998.