Tuesday, 27 January 2015

FAHAMU MAMBO YATAKAYOKUWEZESHA KUISHI KWA FURAHA


Kuna baadhi ya watu wamekuwa wakiishi pasipo kuwa na furaha kwa muda mrefu kutokana na sababu za kimaisha pamoja na magumu wanayoyapitia katika mazingira yao ya kila siku. 


Ni wazi kwamba katika maisha haya kuna wakati mtu unajikuta ukikabiliwa na mambo magumu mbalimbali ambayo mara nyingine hupelekea hata kukata tamaa kabisa ya kuishi,  hivyo kujikuta akiishi pasipo kuwa na furaha kabisa, lakini wataalam wa mambo ya saikolojia wanasema tatizo hili huweza kutatulika kwa kuanza na mhusika mwenyewe anayepitia katika hali hiyo.

Mara nyingi, mtu kuwa na furaha hukutegemea sana na wewe mwenyewe kuliko vitu au watu wengine, lakini hivi sasa kuna baadhi ya watu wanapitia katika hali ngumu ya maisha hadi kufikia hatua ya kushindwa kucheka au kufurahi, lakini hayo yote ni mambo yanayoweza kuchangiwa na wewe mwenywe pamoja na nafsi yako, hivyo ni vizuri ukajaribu kuyazingatia haya machache kwa ajili ya kurejesha furaha yako.

Jenga tabia ya kuwasamehe wanaokukosea
Msamaha ni muhimu kwa sababu hapa duniani hakuna mtu aliyekamilika na hata vitabu vya dini vinatuhamasisha kusameheana pindi tunapokoseana. Inawezekana kuna mtu amekutenda kitu kibaya huenda kwa makusudi au bahati mbaya, lakini kwa ujumla wake tunasema amekukosea. Si vizuri kukaa au kuishi na kisirani kwa sababu ya mtu au watu waliokufanyia ubaya kwa muda mrefu, kwani huweza kukusababishia matatizo ya kiafya (depression) au kuharibu kabisa uhusiano wako na watu uliokosana nao. Kuwa na tabia ya kuyasahau maudhi unayoyapata kwa watu na inapobidi waelewe juu ya makosa yao kuliko kukaa na kisirani.

Anza sasa kuamua kuwa mshindi katika maisha yako
Hii ni ile namna ya kujijengea kwamba wewe unaweza na ni mshindi pia hata kama unapitia mambo magumu kiasi gani, Unapoanza kuwa mshindi wa maisha yako mwenyewe huweza kusaidia kuanza kuwavutia watu wengine na mara utakapopata mafanikio itakusaidia kupata marafiki wazuri, ingawaje miongoni mwao huweza kuwepo marafiki wa kweli na wa uongo. Hakikisha siku zote unachagua kufanya mambo yako kwa uhodari na kujiamini, hata kama baadhi ya watu watakuvunja moyo au kukudharau.

Epuka kuwajali wale wanaokuondolea furaha
Inawezekana kila siku huwa upo karibu na watu ambao kwa namna moja au nyingine huchangia katika kuondoa furaha yako na huenda umekuwa ukijaribu  kuwavumilia na kujikuta unashindwa kabisa basi kama ni hivyo ni vyema ukawapuuza au kama inawezekana kaa nao mbali. Jaribu kutafuta mahali pengine unapoweza kukaa kwa amani na furaha, kwa sababu hakuna haja ya kuendelea kuhuzunika kwa sababu ya mtu au watu fulani ambao wanachangia kuondosha furaha ya maisha yako.


Kuwa mkweli na muadilifu
Tunafahamu kwamba, wengi wetu hatupendi kudanganywa na wala sina uhakika endapo wewe unapenda kudanganywa, hivyo kama wewe hupendi kufanyiwa hivyo basi na wewe usifanye kwa mwingine. Mtu unapokuwa muadilifu matokeo yake watu hukuamini na kukutegemea katika mambo mbalimbali jambo ambalo husaidia kuimarisha furaha ya maisha yako zaidi pia.

Kuwa mkarimu kwa watu wengine
Kumbuka kuwa si watu wote wanaweza kukuona kuwa wewe ni mwema hata utende mambo yaliyo mema maisha yako yote, hivyo jitahidi kuwa mkarimu kwa watu wote bila kujali endapo wanatambua wema wako au hawatambui. Hii husaidia kutojali na kuumia sana pale utakapoona watu hawajachukulia mchango wako kwa uzito ulioutegemea hivyo utaendelea kubaki na furaha yako muda wote.

Hizo ni baadhi ya njia zinazoweza kukusaidia kuwa mtu mwenye furaha maishani mwako ni vizuri ukatambua kuwa furaha ni muhimu sana kwa afya yako, kwani watu waishio pasipo na furaha huweza kuwa katika hatari zaidi ya kupatwa na magonjwa yasiyoambukiza.

No comments:

Post a Comment