Wednesday, 21 January 2015

MANDAI HERBALIST CLINIC NI WADAU WAZURI PIA KATIKA MASUALA YA KIJAMII NA HASA KATIKA ELIMU

Mkuu wa Wilaya ya Ilala, Raymond Mushi (kulia) akimshukuru Dk Abdallah Mandai (kushoto) baada ya kutoa msaada wa madawati katika Shule ya Msingi Mongolandege iliyopo Ukonga jijini Dar es Salaam Mandai Herbalist Clinic ni miongoni mwa wadau wakubwa pia ambao wanathamini sana kuhusu jamii yakiwemo masuala ya elimu, ambayo ni mojawapo ya maeneo muhimu na yanayohitaji vipaumbele sana kutokana na kuwa na  umuhimu wake katika maendeleo ya jamii pamoja na Taifa kwa ujumla.


Dk Abdallah Mandai ambaye ni Mkurugenzi Mkuu wa kituo hicho anasema kwamba, sekta hiyo ni muhimu kwa sababu ni sekta ambayo mara zote hutarajiwa kuzalisha wataalam wa kada mbalimbali kuanzia elimu ya awali hadi elimu ya juu.

Dk Mamdai anaeleza kwamba, ni wazi kuwa sekta hii ya elimu imekuwa ikikabiliwa na changamoto mbalimbali katika baadhi ya shule za hapa nchini na miongoni mwa changamoto hizo ni pamoja na uhaba wa vitabu na vyumba vya madarasa, vyoo pamoja na uhaba wa madawati, suala ambalo limekuwa likichangia wanafunzi kusoma wakiwa wamekaa chini na hata kupelekea ufaulu kushuka wakati mwingine.

Mara zote jamii imekuwa ikiamini kwamba changamoto kama hizo zinazoikabili sekta hiyo ya elimu ni serikali ndio yenye jukumu la kushughulikia changamoto kama hizo, lakini Dk Mandai anasema kwamba masuala kama hayo yanaweza kutatuliwa na jamii pia kwani wanajamii nao wana nafasi yao katika kuchangia masuala muhimu kama hayo ya elimu.

“Jamii inapaswa kujenga utamaduni wa kujitolea hasa katika maendeleo yanayohitaji nguvu ya pamoja kama vile elimu,” alisema Dk Mandai.

Kwa kulitambua hilo Dk Mandai kupitia kliniki yake ya Mandai Herbalist Clinic mwishoni mwa mwaka 2014 alikabidhi msaada wa madawati 20 katika Shule ya Msingi Mongolandege, iliyopo Ukonga jijini Dar es Salaam ikiwa ni moja ya kuirejeshea jamii kwa kile alichobarikiwa na mwenyezi Mungu.

Dk Mandai alisema kuwa, jamii inatakiwa kushirikiana katika mambo ya elimu ili kufanikisha kuleta maendeleo na kujenga utamaduni wa kujitolea hasa katika maendeleo yanayohitaji nguvu ya pamoja kama vile elimu. 
Dk Abdallah Mandai na Mkuu wa Wilaya ya Ilala Raymond Mushi wakiyapanga vizuri madawatiAidha, katika makabidhiano hayo ya madawati ambayo yalishuhudiwa na Mkuu wa Wilaya ya Ilala Raymond Mushi, ambaye alisema kwamba ni vizuri watu wakaiga mfano wa Dk Mandai.

“Watu wanatakiwa kuiga mfano kama wa Dk Mandai ambaye anaonesha moyo wake wa kuliletea Taifa maendeleo na hii ni vizuri ikawa changamoto kwa wengine katika jamii,” alisema Mushi.

Mushi aliendelea kusema kwamba, katika masuala ya elimu kila mtu anatakiwa kuchangia maendeleo kidogo na sio kila kitu kuiachia serikali pekee, kutokana na serikali kushughulikia vitu mbalimbali, huku akiongeza kuwa jamii inapaswa kuhakikisha vijana wanafikia viwango vya kimataifa kwa  kujengewa uwezo.

Sambamba na hayo, mkuu huyo wa wilaya alimpongeza sana Dk Mandai kwa kuwapatia wanafunzi msaada huo wa madawati, huku akisema madawati hayo yatasaidia kupunguza idadi ya wanafunzi kukaa sakafuni, na kuwasihi wanajamii wenye mapenzi mema na nchi yetu kuendelea kusaidia katika sekta hiyo.

Naye Mwalimu Mkuu wa Shule hiyo, Hamis Omary alibainisha kwamba shule hiyo imekuwa ikikabiliwa na changamoto nyingi ikiwemo ya kutokuwa na vyumba vya madarasa, vyoo, ofisi na madawati. Huku naye pia akiwaomba wanajamii, wahisani na wafadhili wawasaidie madawati mengine ili kuweza kuwasaidia wanafunzi kusoma, huku wakiwa wamekaa katika madawati.

No comments:

Post a Comment