Tuesday, 27 January 2015

PRESHA NI UGONJWA UNAOCHANGIWA NA MAISHA TUNAYOISHI KILA SIKU

Ugonjwa wa shinikizo la juu la damu au presha ugonjwa ni moja ya magaonjwa yanayopatikana katika kundi la magonjwa yasiyoambukiza na mara nyingine ugonjwa huu umekuwa ukiitwa kama muuaji wa kimya kimya (Silent Killer)


Ugonjwa huu umefananishwa na muuaji wa kimya kimya  kwa maana kuwa, mtu anaweza kuwa na ugonjwa huu kwa miaka kadhaa, lakini bila kujua, huku ugonjwa huo ukimletea madhara makubwa.

Kwa mujibu wa Shirika la Afya Duniani (WHO) linabainisha kuwa ugonjwa wa shinikizo la damu la juu unakadiriwa kusababisha vifo vya watu milioni 7.5, ambayo ni sawa na asilimia 13 ya jumla ya vifo vyote duniani.

Pia taarifa kutoka shirika hilo zinasema kuwa, kati ya watu wazima watatu duniani, mmoja huwa na tatizo la shinikizo la juu la damu, huku kwa upande wa Afrika WHO inaeleza kuwa zaidi ya asilimia 40 hadi 50 ya watu wazima wanakadiriwa kuwa na tatizo la shinikizo la damu na inaelezwa kiwango hicho kinaweza kuongezeka zaidi.  

Mtaalam wa tiba asili kutoka Mandai Herbalist Clinic anasema Shinikizo la damu kwa kawaida huchangiwa na kuongezeka kwa msukumo wa damu katika kuta za mishipa ya damu, hali ambayo huufanya moyo kufanya kazi zaidi kuliko ilivyo kawaida yake, huku lengo likiwa ni kuweza kuzungusha damu mwilini. 

Kwa kawaida shinikizo la damu la mtu hupanda na kushuka kila siku, lakini baadhi ya watu hubakia juu na hapo ndipo mtu huweza kuambiwa anashinikizo la juu la damu.

Aidha, mtaalam Dk Mandai anasema kuwa shinikizo la damu huweza kupelekea mifumo mingine ya mwili kuharibika, ambayo ni pamoja na figo kushindwa kufanya kazi vizuri, mhusika kupatwa na maradhi ya kiharusi au shambulio la moyo.

Kwa kawaida shinikizo la damu ni muhimu kwa ajili ya kusukuma damu katika sehemu zote za mwili. Kiwango cha shinikizo la damu cha kawaida ni 120 mm Hg1 wakati moyo unapodunda (systolic)  na moyo unapokuwa umepumzika (diastolic) kiwango cha shinikizo la damu hupaswa kuwa 80 mmHg1, hivyo inapozidi au kupungua zaidi ya hapo huweza kuwa tatizo.

Lakini pia mtu anaweza kuwa katika hali ya kawaida endapo presha yake itakuwa katika 140 kwa 90.

Mtaalam huyo anafafanua kuwa, kimsingi kuna aina nyingi za tatizo la shinikizo la damu, lakini kubwa zaidi zimegawanyika katika makundi mawili, ambayo ni shinikizo la damu la‘primary / essential hypertension,’ ambapo aina hii ya shinikizo la damu la juu huwapata asilimia 90 hadi 95 na huwa hawana chanzo cha kitabibu kinachofahamika. Ingawa aina hii ya shinikizo la damu huwa haina chanzo cha moja kwa moja.

Sababu zinazoelezwa kuchangia aina hii ya kwanza ni pamoja na zile za kijenetiki na za kimazingira kama chakula na mazoezi huwa na nafasi kubwa  katika usababishaji wa ugonjwa huo. Hivyo mambo haya yafuatayo yamekuwa yakihusishwa katika kusababisha aina hii ya shinikizo la damu ikiwa ni uvutaji sigara, unene, unywaji pombe, upungufu wa madini ya potassium, kurithi, umri mkubwa, chumvi na madini ya sodium kwa ujumla, ongezeko la kemikali kwenye figo na kushindwa kufanya kazi kichocheo cha insulin.

Asilimia 5 hadi 10 ya ugonjwa wa shinikizo la damu husababishwa na shinikizo la damu aina ya pili, ambayo huitwa ‘secondary hypertension.’ Aina hii ya pili husababishwa na tatizo lililopo mwilini. Matatizo hayo ni pamoja na kasoro ya kuzaliwa nayo katika mshipa mkubwa wa damu, saratani ya figo, saratani ya tezi iliyo juu ya figo, hali ya kushindwa kupumua vyema usingizini (sleep apnea,) ujauzito ambapo baadhi ya akina mama wajawazito hupata shinikizo la damu suala linalosababisha hatari ya kupata kifafa cha mimba (eclampsia) na pia magonjwa ya figo kama vile mshipa wa damu wa figo kuwa mwembamba pamoja na matumizi ya baadhi ya madawa ya kulevya au kemikali n.k.

Dk Mandai anabainisha baadhi ya sababu  zinazochangia kupata shinikizo la damu, ikiwa ni pamoja na umri mkubwa, ukosefu wa mazoezi, msongo wa mazoezi, matumizi ya pombe kupita kiasi, matumizi ya chumvi yaliyokithiri, unene kupita kiasi, uvutaji wa sigara pamoja na historia ya ugonjwa katika familia n.k

Mtaalam huyo anasema makundi ambayo wapo katika hatari ya kupata ugonjwa huu ni pamoja na watu wenye ndugu ambao waliwahi kuwa na tatizo hilo, wenye umri zaidi ya miaka 35, kinamama wajawazito, wale ambao wanakula vyakula vyenye mafuta mengi pamoja na chumvi nyingi watumiaji wa pombe  kupita kiasi, wavutaji wasigara, wale wenye mazoezi hafifu pamoja na watu wenye unene kupita kiasi. n.k.

Hata hivyo, mtaalam huyo anasema ugonjwa huo hauna dalili za jumla ndio maana huitwa muuaji wa kimya kimya, lakini mgonjwa huweza kuhisi kizunguzungu, kuumwa kichwa, kupata kichefuchefu na kutapika, lakini wengine hupatwa na maumivu ya kifua na kushindwa kupumua. Hivyo ni vizuri kujenga tabia ya kupima mara kwa mara ili kujua endapo una tatizo.

Pamoja na hayo, Dk Mandai anasema unaweza kuepuka tatizo hili kwa kula lishe bora yenye matunda na mbogamboga pamoja na chakula kisichokuwa na mafuta mengi.  
Sambamba na hayo, ni vyema kupenda  kufanya mazoezi mara kwa mara, angalau nusu saa kwa siku na ikiwa wewe ni mtumiaji wa sigara au pombe ni vizuri ukajitahidi kuacha, huku njia nyingine ikiwa ni kupunguza matumizi ya chumvi nyingi katika chakula hasa ya kuongeza mezani pamoja na kuondokana na msongo wa mawazo. 

Pia unaweza kukutana na Dk Mandai kutoka Mandai Herbalist Clinic kituo ambacho kinapatikana Ukonga, Mongolandege jijini Dar es Salaam na utapata tiba ya maradhi mbalimbali yakiwemo na yale sugu kwa kutumia dawa asilia za mimea na matunda zisizo na kemikali.

No comments:

Post a Comment