Advertisement

Advertisement

.

.

Mixer

Mixer

Monday, 19 January 2015

UGONJWA WA EBOLA WAELEZWA KUPUNGUA


Waziri wa Afya wa nchini Mali, Ousmane Kone, ametangaza kuwa nchi hiyo kwa sasa haina maambukizi ya virusi vya Ebola, hii ni baada ya siku 42 za kutokuwa na wagonjwa wapya walioambukizwa virusi vya ugonjwa huo.

Waziri huyo alisema
"natangaza siku hii, mwisho wa ugonjwa wa virusi vya Ebola nchini Mali," huku akibainisha kwamba mtu wa mwisho kuambukizwa Ebola nchini humo alipona na kuruhusiwa kutoka hospitali mapema mwezi Disemba mwaka jana.
Taarifa zinasema kwamba, takwimu za hivi karibuni zinaonesha kuwa nchi tatu za Afrika magharibi zilizokuwa zimeathirika zaidi zote zimeshuhudia kupungua kwa wagonjwa wapya wa Ebola.

Mbali na hayo, pia Sierra Leone na Guinea zote zimekuwa na jumla ya chini kabisa ya wagonjwa waliothibitika kila wiki kuambukizwa virusi vya Ebola tangu mwezi Agosti, kwa mujibu wa takwimu za Umoja wa Mataifa zilizotolewa hivi karibuni.

Pia nchi ya Liberia, nayo  haikuripoti wagonjwa wapya kwa muda wa siku mbili wiki iliyopita, lakini nayo pia ilikuwa na idadi ya chini kabisa ya wagonjwa kwa wiki ya mambukizi ya Ebola tangu mwezi Juni.

Pamoja na hayo, inaelezwa kwamba idadi ya watu waliofariki kutoka na virusi vya Ebola imefikia watu 8,429, huku 21,296 wakiwa wameambukizwa.

Hali kadhalika nchi ya Mali iliandikisha mgonjwa wa kwanza wa Ebola mwezi Oktoba, wakati mtoto wa miaka miwili kutoka Guinea alipougua na kufariki na itakumbukwa kwamba katika kipindi cha hali mbaya kabisa ya ugonjwa wa Ebola nchini humo watu 300 waliwekwa chini ya uchunguzi kuhusiana na maambukizi ya virusi vya Ebola. Lakini nchi hiyo kwa sasa imeepukana na ugonjwa huo, alisema Ibrahima Soce Fall, Mkuu wa Ofisi ya Umoja wa Mataifa nchini Mali kuhusu Ebola (UMEER).

Wataalam wa afya wanasema kwamba ugonjwa wa Ebola huchukua siku 21 tangu mtu anapoambukizwa hadi kujitokeza kwa dalili za ugonjwa huo na taratibu za nchi kutangaza kuwa zimeondokana na maambukizi ya ugonjwa Ebola ni lazima zisiwe na wagonjwa wapya kwa vipindi viwili vya matazamio yaani siku 42.

No comments:

Post a Comment