Wednesday, 4 February 2015

DK SEIF:TUNAMPANGO WA KUANZA KAMPENI YA KUPIMA SARATANI YA TEZI DUME BUREIkiwa leo ni siku ya Saratani duniani Serikali imesema inaandaa kampeni ya kuwapima bure wagonjwa wa saratani ya tezi dume.

Hayo yalibainisha mjini Dodoma na Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii Dk Seif Rashid, alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari, ambapo alisema kuwa, upimaji huo utafanyika kama sehemu ya kukabiliana na ugonjwa huo.

Mazungumzo hayo ya Dk Rashid yanakuja kutokana na kuzungumzia maadhimisho ya siku ya Saratini Duniani ambayo hufanyika Februari 4 kila mwaka, ambapo alibainisha kuwa katika kuadhimisha siku hiyo, wizara yake kwa kushirikiana na Taasisi ya Saratani ya Ocean Road ya Dar es Salaam watatoa ujumbe kwa wananchi wote ukielezea namna watakavyoweza kushirikiana kutoa elimu zaidi kwa umma kuhusu maradhi hayo.

Pamoja na hayo, waziri huyo alisema pia watawapima wananchi saratani ya shingo ya kizazi na matiti, lakini pia wizara imeandaa kampeni ya uchunguzi wa sarati ya tezi dume itakayofanyika mapema mwaka huu.

Hata hivyo, alibainisha kuwa tarehe kamili ya kuanza kufanyika kwa uchunguzi huo itatangazwa pindi mipango itakapokamilika na upimaji huo utafanyika bure.

Sambamba na hayo, Dk Rashid alisema maradhi ya saratani yamekuwa yakiongezeka kila siku duniani ingawa idadi kubwa ya wagonjwa iko katika nchi zinazoendelea.

"Kwa mujibu wa Shirika la Afya Duniani (WHO) kila mwaka wagonjwa wapya milioni 12.6 hugundulika duniani wakiwa na saratani, huku hapa nchini idadi ya wagonjwa wapya wa saratani kila mwaka ni 34,000, lakini wengi wao hawafiki hospitali kutokana na sababu mbalimbali" alibainisha Dk Rashid

No comments:

Post a Comment