Advertisement

Advertisement

.

.

Mixer

Mixer

Monday, 9 March 2015

HII NI SIMANZI MTOTO MWINGINE MWENYE ULEMAVU WA NGOZI (ALBINO) AKATWA KIGANJA CHA MKONO


Matukio ya ukatili dhidi ya walemavu wa ngozi (albino) yameendelea kuwa tishio hapa nchini baada ya mtoto wa miaka sita kukatwa kiganja cha mkono.


Tukio hilo limetokea mkoani Rukwa, wilayani Sumbawanga baada ya mtoto Baraka Cosmas (6) ambaye anaishi na wazazi wake katika kijiji cha Kipeta, Bonde la ziwa Rukwa kukatwa kiganja

Mtoto Baraka alishambuliwa na kujeruhiwa vibaya na watu wasiojulikana kwa kumkata kiganja cha mkono wake wa kulia na watu wasiojulikana kisha kutokomea kusikojulikana.

Kwa upande wa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Rukwa Jackob Mwaruanda alisema tukio hilo la kikatili lilitokea saa saba usiku wa kuamkia juzi.

Alisema wakati hayo yalipokuwa yakitokea baba mzazi wa mtoto huyo anadaiwa alikuwa amelala katika nyumba ya mkewe mdogo kijijini humo.

Kamanda Mwaruanda alisema mtoto huyo amelazwa katika kituo cha  Afya cha Kamsamba wilayani Momba mkoani Mbeya kwa matibabu akiwa pamoja na mama yake mzazi.

Hata hivyo Kamanda Mwaruanda alisema kuwa watu watatu majina yao yamehifadhiwa wanashikiliwa na polisi na uchunguzi zaidi kuhusiana na tukio hilo unaendelea ili kuwasaka wahusika na kiungo cha mtoto huyo.

Mama mzazi Prisca Shaabani (28) alisema tukio hilo lilitokea saa saba usiku alipokuwa akitaka kutoka nje kujisaidia.

“Nilikutana na mtu akifungua mlango, akanipiga na kitu kichwani kisha nikazimia nilipozinduka nikapiga kelele na majirani wakafika ndipo nilipogundua mtoto wangu amekatwa kiganja cha mkono wa kulia” alisema mama mzazi.

Tukio hilo limetokea wakati serikali ikiwa katika mkakati kabambe wa kupambana na mauaji ya albino na ikiwa ni wiki chache tangu mtoto Yohana Bahati aliyekuwa na umri wa mwaka mmoja alipotekwa Februari 15, mwaka huu na kukutwa ameuawa katika eneo la Shilabela.

Hali kadhalika shambulio hilo linajitokeza wiki moja tu baada ya watuhumiwa wanne kuhukumiwa adhabu ya kifo kwa mauaji ya albino, Na muda mfupi baada ya Rais Tanzania Jakaya Kikwete kukemea mauaji ya albino, ambao viungo vyao hutumika katika shughuli za kishirikina kwa imani potofu kuwa zinasaidia kuleta utajiri na madaraka.

Mandai Herbal Clinic tunatoa rai kwa Wananchi wote kushirikiana kwa pamoja katika kukabiliana na mauaji ya ndugu zetu hawa wneye ulemavu wa ngozi na kuwasihi watu wanaoshiriki katika mauaji haya kuachana na tabia hiyo kwani hakuna ukweli wowote juu ya viungo hivyo kuwa chanzo cha utajiri kwani nao ni binadamu kama walivyowengine.Kwa pamoja tushirikiane kutokomeza mauaji haya.

No comments:

Post a Comment