Thursday, 23 April 2015

AJALI ZAENDELEA KULILETEA TAIFA MAJONZI, WATU 10 WENGINE WAPOTEZA MAISHA KATIKA AJALI NAKUSABABISHA MAJERUHI 51
Ajali zimeendelea kusababisha majonzi kwa Watanzania baada ya watu 10 kufariki katika ajali mkoani Shinyanga.


Katika ajali ya jana, watu tisa walifariki dunia papo hapo na mmoja kupoteza maisha mara baada ya kufikishwa hospitalini.

Ajali hiyo ilitokea jana saa 8:45 mchana katika kijiji cha Samuye, Shinyanga vijijini, baada ya basi la kampuni ya Unique namba T148 BKK aina ya Scania kukutana uso kwa uso na tela la lori la kampuni ya Coca – Cola. Tela hilo lenye namba T635 AJT katika barabara kuu ya Shinyanga - Nzega.

Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Shinyanga, Justus Kamugisha, alisema ajali hiyo ilitokana na lori la kampuni ya Coca - Cola lililokuwa na tela kulipita gari lingine, lakini kabla tela halijaingia katika barabara yake, lilikutana na basi hilo lililokuwa katika mwendo kasi na kusababisha ajali hiyo.

“Ni watu 10 waliopoteza maisha katika ajali hiyo, lakini wengine 51 wamejeruhiwa vibaya na kukimbizwa katika Hospitali ya Mkoa wa Shinyanga kupatiwa matibabu,” alisema Kamanda Kamugisha.

Naye Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Mkoa wa Shinyanga, Dk. Salum Mfaume, alithibitisha kupokea miili tisa huku mtu mmoja akifariki dunia hospitalini hapo wakati akipatiwa matibabu pamoja na majeruhi 51.

“Kweli tumepokea miili tisa ya watu waliokufa katika ajali, lakini mtu wa 10 alifariki dunia wakati akipatiwa matibabu, pia tuna majeruhi wengine 51 walionusurika kutokana na ajali ya basi hilo,” alisema Dk. Mfaume.

Mungu azilaze roho za marehemu mahala pema peponi Amen, na Mwenyezi Mungu awajaalie nafuu ya haraka majeruhi wote.
 

No comments:

Post a Comment