Wednesday, 15 April 2015

RADI YAKATISHA NDOTO ZA WANAFUNZI NI BAADA YA KUPIGA NA KUSABABISHA VIFOMoja ya habari kubwa leo April 15, 2015 hapa nchini ni taarifa kuhusu watu nane wakiwemo wanafunzi sita wa shule ya msingi Kibirizi katika Manispaa ya Kigoma kufariki  dunia baada ya kupigwa na radi kufuatia mvua kubwa iliyokuwa ikinyesha kuanzia jana asubuhi hadi mchana.


Taarifa iliyotolewa na Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Mkoa Kigoma ya Maweni, Fadhili Kibaya alisema sambamba na watu hao waliofariki pia watu 15 walijeruhiwa katika tukio hilo.

Dk Kibaya amewataja waliokufa kuwa ni pamoja na Yusuf Athuman, Hassan Ally, Fatuma Sley, Zamda Seif, Shukrani Yohana na Warupe Kapupa ambao ni wanafunzi wa darasa la kwanza katika shule hiyo ambapo Mwalimu aliyefariki ametambuliwa kwa jina la Elieza Mbwambo aliyekuwa akifundisha darasa la tano.

Mbali na watu hao mtu mwingine aliyetambuliwa kwa jina la Focas Ntahamba naye alifariki katika eneo la Bangwe, Manispaa ya Kigoma -Ujiji kwa kupigwa na radi kufuatia mvua hiyo ambapo mganga huyo alisema kuwa watu 10 kati ya 15 waliojeruhiwa katika tukio hilo walipatiwa matibabu na kuruhusiwa kurudi nyumbani.

Hata hivyo, mmoja wa walimu wa Shule ya Msingi Kibirizi, Wilbert Emmanuel ambaye alikuwepo eneo la tukio alisema wamesikitishwa na tukio hilo ambalo lilitokea bila kutegemea na kuacha simanzi kubwa shuleni hapo.

Mwalimu Emmanuel alisema kuwa sehemu kubwa iliyoathiriwa ni darasa la kwanza ambapo Mwalimu aliyefariki alikutwa na mauti hayo akiwa katika ofisi ya walimu akiwa na walimu wenzake.

Mmoja wa walimu waliojeruhiwa katika tukio hilo, Menina Sililo ambaye alikuwa akifundisha darasa la kwanza ambalo limeathiriwa zaidi na janga hilo alisema wakati mvua inanyesha alikuwa akiendelea kufundisha na baada ya mvua kuongezeka na giza kutanda aliacha kufundisha na kuwataka wanafunzi kukaa na kutulia.

Alisema baada ya muda alisikia kishindo kikubwa na kujikuta akirushwa sakafuni huku miale ya radi ikiwa imetanda darasa zima na sehemu kubwa ya wanafunzi wakipiga kelele kuomba msaada ambapo alijikongoja na kutoka nje ya darasa kuomba msaada huo kwa waliokuwa jirani.

Mwalimu Sililo alisema katika tukio hilo amejeruhiwa mguu na mkono wa kulia na kwamba anamshukuru Mungu hakupata majeraha makubwa.

Pole za dhati ziwafikie wakazi wa Kigoma na Watanzania kwa ujumla kufuatia tukio hilo, Mwenyezi Mungu awapumzishe kwa amani marehemu wote na kuwapa nguvu wapendwa wote wa marehemu.

No comments:

Post a Comment