Thursday, 23 April 2015

RIPOTI ILIYOTOLEWA NA SHIRIKA LA AFYA ULIMWENGUNI KUHUSU EBOLA IPO HAPAShirika la Afya Duniani (WHO) limetangaza kuwa, zaidi ya watu 26,000 wameambukizwa virusi vya homa hatari ya Ebola tangu ugonjwa huo ulipoibuka mwishoni mwa mwaka 2013. 


Taasisi hiyo ya Umoja wa Mataifa imebainisha katika ripoti yake ya hapo jana kwamba, watu 26,079 wameambukizwa virusi vya Ebola, huku wengi wao wakiwa ni raia wa nchi tatu za Kiafrika za Liberia, Guinea na Sierra Leone tangu virusi hivyo vilipoibuka Disemba mwaka 2013. 

Aidha, ripoti hiyo ya WHO imeeleza kuwa, 10,823 kati ya walioambukizwa wameshafariki dunia, huku taarifa zaidi zikisema kuwa, kiwango cha maambukizi ya virusi hivyo kimepungua kutokana na watu 33 tu kuripotiwa kuambukizwa virusi hivyo kwa wiki.

Liberia ambayo ni miongoni mwa nchi zilizoathiriwa zaidi na virusi vya Ebola, haijaripoti kesi mpya ya kupoteza mtu maisha kwa homa hiyo tangu mgonjwa wa mwisho aage dunia mwezi uliopita wa Machi. 

Mwezi ujao wa Mei Liberia inataraji kutangaza kutokomezwa maradhi hayo nchini humo endapo hakutaripotiwa kesi mpya ya maambukizi. 

Ikumbukwe kwamba dalili za Ebola ni homa kali, kuharisha, kutapika na kutokwa damu katika sehemu mbalimbali mwilini.

Mtu anaweza kuambukizwa ugonjwa huo kwa kugusa kinyesi na majimaji ya aina zote yanayotoka kwa mgonjwa kama vile damu, mate na hata jasho.

No comments:

Post a Comment