Advertisement

Advertisement

.

.

Mixer

Mixer

Thursday, 30 April 2015

SERIKALI YAWASILISHA MUELEKEO WA BAJETIWaziri wa Fedha Saada Mkuya Salum


Serikali imewasilisha mwelekeo wa bajeti kwa Kamati ya Bunge, ambayo inalenga zaidi kupeleka umeme na huduma za maji vijijini, kumalizia miradi ambayo haijakamilika na kutenga fedha kwa ajili ya uchaguzi mkuu ujao.


Waziri wa Fedha, Saada Mkuya Salum alisema wanaandaa bajeti ambayo itasaidia kumaliza mambo yote waliyoahidi, ambayo yameainishwa kwenye Ilani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), ambayo serikali iliahidi wakati wa kampeni za uchaguzi mkuu uliopita.

Hata hivyo waziri huyo alisema “bajeti ya mwaka 2015/16 ni ya kipekee. Ni mwaka wa uchaguzi, ni mwaka ambao serikali ya Awamu ya Nne inamaliza muda wake na serikali mpya kuingia madarakani. “Ni mwaka ambao Mkukuta na Mpango wa Kwanza wa Maendeleo ya Milenia ya miaka mitano inafikia tamati, Malengo ya Milenia ya mwaka 2015 yanafikia ukomo na pia utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi ya mwaka 2010 unakamilika,”

Aidha, akiwasilisha mwelekeo wa bajeti hiyo kwa wabunge jijini Dar es Salaam jana, Mkuya alisema bajeti ya mwaka huu imelenga zaidi kutathmini na kuangalia changamoto kwenye sekta ya maji, nishati, rasilimaliwatu na kumalizia miradi ambayo haijakamilika.

“Vipaumbele kwenye bajeti hii vimejikita zaidi kwenye kuandaa awamu ya pili ya Mpango wa Maendeleo wa miaka mitano utakaoanza Juni mwaka 2016, na mkazo zaidi ni kwenye miradi ya umeme vijijini, maji vijijini, kuimarisha rasilimaliwatu na kugharamia uchaguzi mkuu,” alisema Mkuya.

Akieleza zaidi Mkuya alisema katika mwelekeo huo wa Bajeti mpya ya mwaka 2015/16, jumla ya Sh takribani trilioni 23 zinatarajiwa kukusanywa na kutumika katika matumizi ya maendeleo na ya kawaida.

Alisema katika matumizi ya maendeleo, vipaumbele vitano ambavyo ni maji, umeme, rasilimaliwatu na kumalizia miradi viporo na kugharamia uchaguzi mkuu. Jumla ya fedha zilizotengwa ni Sh trilioni 5.8.

Mchanganuo wake ni kwamba fedha za ndani ni Sh trilioni 4.3 na fedha za nje ni Sh trilioni 1.4 ambazo kwa ujumla zitatumika kwenye utekelezaji wa vipaumbele vilivyoainishwa na kumalizia miradi ambayo haikukamilika kwenye bajeti iliyopita.

Katika sekta ya nishati, kipaumbele kimewekwa katika kuendeleza miradi ya umeme vijijini, ambapo hadi sasa wateja 2,602 wa vijijini kwenye mikoa ya Kagera, Tanga. Simiyu, Singida, Iringa na Ruvuma wameunganishiwa umeme.

Mbali na hayo nako katika sekta ya maji vijijini, tathimini ya bajeti iliyopita, inaonesha kuwa jumla ya miradi ya maji vijijini, ilikuwa 123 iliyojengwa na kukamilika na idadi hiyo imewanufaisha wananchi 463,750.

Pamoja na hayo bajeti hii, imeonekana kuweka mkazo katika kukamilisha miradi ya maji vijijini ambayo haijakamilika, ikiwemo miradi ya ujenzi wa mabwawa ya Kawa mkoani Rukwa, bwawa la Mwanjoro lililopo Shinyanga na bwawa la Sasajila lililopo Dodoma pamoja na miradi mingine kwenye maeneo ya vijijini.

Kuhusu suala la Uchaguzi Mkuu, unaotarajiwa kufanyika Oktoba mwaka huu, ambalo ni moja ya vipaumbele katika bajeti hiyo mpya, Mkuya alisema bajeti imejikita katika kugharamia uchaguzi huo ili ufanyike na kupata serikali mpya itakayoendelea kutekeleza bajeti hii.

Mkuya aliendelea kusema kuwa Serikali imepanga kutumia Sh trilioni 22.48 kwa ajili ya matumizi ya kawaida na maendeleo katika bajeti ya mwaka 2015/16 huku utegemezi wa fedha za kigeni ukionekana kupungua kutoka asilimia 14.8 ya mwaka wa fedha uliopita hadi asilimia 8.4 kwa mwaka ujao wa fedha.

Itakumbukwa kwamba bajeti ya mwaka 2014/15 ilikuwa ni Sh trilioni 19.9, hivyo mwelekeo wa bajeti hiyo inakuwa na ongezeko kwa takribani asilimi 16.

Akifafanua zaidi Mkuya alisema katika fedha hizo, sh trilioni 16.71 zimetengwa kwa ajili ya matumizi ya kawaida, ikijumuisha Sh trilioni 6.61 kwa ajili ya mishahara ya watumishi wa Serikali na taasisi, Sh trilioni 3.41 kwa ajili ya matumizi mengineyo ya Wizara huku mikoa ikiwa ni Sh bilioni 83.55 na Mamlaka za Serikali za Mitaa ni Sh bilioni 208.75 wakati Sh trilioni 2.60 zikitengwa kwa ajili ya kulipia hati fungani na dhamana za serikali zinazoiva.

Aidha, Mkuya alisema matumizi ya maendeleo yatakuwa Sh trilioni 5.77 sawa na asilimia 25.9 ya bajeti yote ambapo kiasi cha sh trilioni 4.33 ni fedha za ndani sawa na asilimia 75 ya fedha za maendeleo na trilioni 1.44 fedha za nje.

“Kwa kuzingatia sera za uchumi na misingi ya sera za bajeti, sura ya bajeti inaonesha kuwa Sh trilioni 22.48 zinatarajia kukusanywa, ambapo mapato ya ndani ya Serikali Kuu yanatarajia kuwa Sh trilioni 14.82 ambayo ni sawa na asilimia 57.8 ya bajeti yote."

Alisema serikali inalenga kukusanya mapato ya kodi ya jumla ya Sh trilioni 13.35 sawa na asilimia 90.1 ya mapato ya ndani huku mapato yasiyo ya kodi ni Sh bilioni 949.2 na yale yatokanayo na vyanzo vya halmashauri yanatarajia kuwa Sh bilioni 521.9.

Sambamba na hayo, Mkuya alisema Serikali inategemea kukopa kiasi cha Sh trilioni 5.77 kutoka vyanzo vyenye masharti ya kiabishara huku washirika wa maendeleo wanatarajiwa kuchangia Sh trilioni 1.89 sawa na asilimia 8.4 ya bajeti, ikilinganishwa na asilimia 14.8 ya bajeti ya mwaka 2014/15 ambazo sehemu kubwa ni mikopo ya masharti nafuu.

No comments:

Post a Comment