Saturday, 2 May 2015

RAIS KIKWETE AMEAHIDI KIWANGO CHA MISHAHARA YA WAFANYAKAZI KUONGEZEKA

Rais Jakaya Kikwete ameahidi kuongeza mishahara ya wafanyakazi kuanzia Julai mwaka huu, hadi kufikia kima cha chini cha karibia Sh 315,000.


Rais Kikwete aliyasema hayo alipokuwa akihutubia wananchi waliohudhuria sherehe za Siku ya Wafanyakazi Duniani, zilizofanyika kitaifa kwenye viwanja vya CCM Kirumba jijini Mwanza jana.

Rais Kikwete alisema, “Ongezeko lililoko ni dogo sana lakini si haba. Na mwaka huu tutaongeza mshahara kufikia Sh 315,000 kima cha chini na kama hakitafikia, tutaangalia mahesabu yetu kwa nini, angalau ikaribie hiyo”.

Rais Kikwete alisema serikali imechukua hatua za makusudi za kuongeza mshahara kila mwaka tangu alipoingia madarakani mwaka 2005 ambapo kima cha chini alikuta Sh 65,000 na amekipandisha na sasa kimefika Sh 265,000 ambayo ni zaidi ya mara nne ya kiwango cha awali.

Kwa upande mwingine alisema serikali imeendelea kupunguza kiwango cha kodi wanayotozwa wafanyakazi (PAYE) mwaka hadi mwaka. Alikuta asilimia 18.5 na kimeshuka katika utawala wake na kufikia asilimia 12.

“Na mwaka huu tutapunguza sijui tutafikia asilimia 9 kama mnavyotaka ila tutakapofikia si pabaya,” alisema Kikwete bila kutaja kiwango cha asilimia kitakachopunguzwa.

Mbali na hayo, akizungumzia mshahara katika sekta binafsi, alisema kima cha chini hupangwa na bodi za mishahara za kisekta na kwamba majadiliano yalikuwepo ambayo yalipandishwa kutoka Sh 48,000 hadi Sh 700,000 kulingana na sekta.

No comments:

Post a Comment