Friday, 12 June 2015

BAJETI YA MWISHO, MAFUTA YA TAA, DIZELI NA PETROL BEI JUU, POMBE NA SIGARA SI TEGEMEZI TENA


Waziri wa Fedha Saada Mkuya
Hapo jana Bajeti ya 2015/16, iliwasilishwa na Waziri wa Fedha Saada Mkuya bungeni mjini Dodoma, huku ikionekana kuwa tofauti na bajeti nyingi zilizopita kutokana na bajeti hiyo kutoongeza kodi katika bidhaa za pombe na sigara.

Bajeti hiyo ya mwisho ya Serikali ya awamu ya nne ya Mhe Rais Jakaya Kikwete, safari hii imepandisha kodi katika uingizaji wa bidhaa nchini kwa ajili ya kulinda viwanda na wazalishaji wa ndani na kuongeza ajira.

Aidha, bajeti hiyo pia imeweka kipaumbele katika kugharamia Uchaguzi Mkuu na kuweka msukumo maalum kwenye miradi ya umeme vijijini, maji vijijini pamoja na kukamilisha miradi ya kimkakati inayoendelea na kuwekeza kwenye rasilimali watu.

Bajeti hiyo imeeleza kudhibiti mianya ya matumizi ya fedha za Serikali na kupunguza misamaha ya kodi, huku ikiwakumbuka wastaafu kwa kuwaongezea mafao ya mwezi kutoka Sh50,000 hadi Sh85,000 pamoja na kupunguza Kodi ya Malipo ya Kadri ya Mapato (Paye) kwa asilimia moja na kuanzisha mafao ya kila mwezi kwa wazee.

Waziri Mkuya pia aliliomba bunge liridhie mabadiliko katika Sheria ya Mafuta ya Petroli Sura namba 392 ili kuongeza tozo ya mafuta ya petroli na dizeli kutoka Sh50 hadi Sh100. Huku tozo ya mafuta ya taa nayo ikiwa imependekezwa kuongezwa kutoka Sh50 hadi Sh150 ikiwa ni moja ya njia ya kupunguza uwezekano wa uchakachuaji.

“Hatua ya kuongeza Tozo ya Mafuta ya Petroli inatarajiwa kuongeza mapato ya Serikali kwa kiasi cha Sh139.78 bilioni na fedha zote zitaelekezwa katika mfuko wa Rea kwa ajili ya utekelezaji wa mradi wa usambazaji umeme vijijini,” alisema Mkuya.

Pia, Mkuya alipendekeza mabadiliko katika Sheria Tozo za Mafuta na Barabara namba 220 ili kuongeza tozo katika mafuta ya Dizeli, Petroli na kwa Sh50 hadi kufikia Sh313. Huku akisema kuwa hatua hiyo ya kuongeza tozo hiyo itaongeza mapato kwa takribani Sh136.4 bilioni ambayo alisema yataelekezwa katika mradi wa kusambaza umeme vijijini wa Rea.

Kuhusu kupunguza kiwango cha chini cha kutoza kodi ya mapato ya ajira kutoka asilimia 12 hadi asilimia 11 alisema hiyo ni dhamira ya Serikali tangu mwaka mwaka 2006/07 kodi hiyo ilipokuwa asilimia 18.5.

Pia, bajeti hiyo inabana uingizaji wa mchele, sukari na vyuma kwa kuongeza ushuru huku bidhaa za nyuzi za kutengezea nyavu, malighafi za kutengenezea pasta na tambi zikiondolewa kodi.

Shukrani kwa kuichagua tovuti hii kupata taarifa mbalimbali, tafadhali endelea kuwa karibu nasi kwa habari mbalimbali, lakini pia ikiwa unasumbuliwa na magonjwa sugu kumbuka Mandai Herbalist Clinic tupo kwaajili yako. Tunapatikana Ukonga, Mongolandege jijini Dar es Salaam. Au tupigie simu namba 0716 300 200, 0754 391 743, 0784 300 300. Barua pepe, dkmandaitz@gmail.

No comments:

Post a Comment