Tuesday, 9 June 2015

DAWA MPYA ZA ARV KWA WATOTO SASA KUCHANGANYWA KWENYE CHAKULA


Watoto walioathirika na Virusi vya Ukimwi watanufaika kutokana na uamuzi wa Mamlaka ya Chakula na Dawa ya Marekani kuidhinisha dawa mpya ambazo zinaweza kuchanganywa kwenye Chakula ili kuwarahisishia matumizi watoto wanaoishi na virusi hivyo.

Hayo yamesemwa na Shirika la Umoja wa Mataifa la kushughulikia Ugonjwa wa Ukimwi ,UNAIDS na Shirika linalohudumia watoto duniani, UNICEF.

Wakielezea juu ya mpango huo Mkurugenzi mtendaji wa UNAIDS, Michel Sidibe' amesema dawa hizo ni mbadala wa zile ambazo zilikuwa hazifurahiwi na watoto, huku zikiwa na ladha mbaya, lakini hizi dawa zitawawezesha watoto kuzidi kupata tiba nzuri na kuwafanya watoto wawe na afya.

Aidha, amesema kuwa dawa hizo zimetengenezwa nchini India na zina viambata vya Lopinavir na ritonavir ambavyo vinauwezo wa kuchanganywa kwenye chakula cha mtoto bila kuharibiwa na joto la chakula na zina ladha nzuri kuliko zinazopatikana sasa.

Naye Mkurugenzi wa Mradi wa Ukimwi wa UNICEF, Craig McClure amesema '' tunatarajia kuimarisha upatikanaji wa matibabu kwa ajili ya watoto wengi zaidi na kuunga mkono mpango wa kuwafikia watoto wasiopata huduma hii duniani kote''.

Pamoja na hayo imeelezwa kuwa hatua hiyo ni mpya katika mipango ya kuokoa maisha ya watoto waishio na virusi vya ukimwi.

No comments:

Post a Comment