Tuesday, 23 June 2015

HIVI UMESIKIA HII TAARIFA YA WAUWAJI WALIOPEWA JINA LA 'WAKATA MAKOROMEO'?


Mwandishi: Goodluck Ngowi,  
Kagera
Wauaji waliobatizwa jina la 'wakata makoromeo' huko mkoani Kagera katika Wilaya ya Missenyi wamewaua watu wawili katika kata ya Gera mwishoni mwa wiki (Ijumaa) kwa kuwakata shingo.

Kwa mujibu wa Jeshi la Polisi wilayani humo, waliouwa ni Gosbert Paschal (50) na Nurdin Nuru (41), wote wakazi wa kijiji cha Katale katika kata hiyo.

Imeelezwa kuwa tukio hilo la mauaji lilifanyika majira ya saa nne usiku ambapo wananchi walizitilia shaka pikipiki mbili zilizokuwa zikizunguka katani humo kwenye barabara ya Gera-Ishozi na Gera-Bwanjai, ambapo moja ya pikipiki hizo ilikuwa na watu wawili na nyingine watatu ambao hawakuwa wanafahamika vizuri.

Baada ya askari Polisi kupata taarifa za kuwapo kwa watu hao, walianza kufukuzana nao bila mafanikio, ndipo baadaye alionekana Paschal akiwa amekatwa panga shingoni upande wa nyuma na upande wa jicho na alikimbizwa katika Hospitali Teule ya Mugana na baadaye kuhamishiwa Hospitali ya Mkoa wa Kagera ambako alifariki kesho yake.

Naye Nururdin yeye alipatikana akiwa amefariki dunia siku ya Jumamosi kando ya barabara, huku naye akiwa amekatwa kwa panga nyuma ya shingo, huku kukiwa hakuna michuruziko ya damu jambo linaloashiria kuwa huenda damu yake ilikingwa.

Hata hivyo, inaelezwa kuwa iwapo wananchi wasingetoa taarifa hizo mapema huenda mauaji yangekuwa zaidi ya hapo kwani baadhi ya watu walikuwa wakitoka kwenye harusi, huku wengine wakiwa wamekunywa pombe.

Kufuatia matukio hayo, Jeshi la Polisi linaendelea na upelelezi mkali na limewataka wananchi kuchukua tahadhari ikiwamo ya kutotembea mtu mmoja mmoja usiku wala sehemu za mbugani.

Unaweza kuendelea kupata taarifa mbalimbali kutoka kwetu www.dkmadai.com kila siku kutoka kwa waandishi wetu waliopo mikoani.

No comments:

Post a Comment