Wednesday, 24 June 2015

KAMBI YA WAZEE NA WALEMAVU WASIOJIWEZA YAKABILIWA NA NJAA MKOANI MWANZA


Goodluck Ngowi
Mwanza
Kambi ya wazee wasiojiweza na walemavu iliyopo Bukumbi Wilayani Misungwi mkoani Mwanza inakabiliwa na wimbi la njaa, huku wakidaiwa shilingi mil 436 kutoka kwa wazabuni mbalimbali.

Akizungumza hapo jana na mwandishi wetu www.dkmandai.com kutoka mkoani humo, Ofisa Mfawidhi wa kambi hiyo, Marco Stansilous, amesema kuwa tangu serikali isitishe kuwapa fedha amekuwa wakikopa chakula kutoka kwa wazabuni.

“Tangu Julai 2013 tunakopa chakula kwa wazabuni sasa tangu mwezi Disemba mwaka jana wahisani wamesitisha kutupa chakula na hatuna fedha yoyote,” alisema Stansilous.

Aidha, Stansilous aliongeza kuwa kambi hiyo kwa sasa haina huduma za afya za kutosha kuwahudumia wazee hao kutokana na kituo cha afya kilichopo katika eneo hilo pia kutumika kuwahudumia wanakijiji wa eneo hilo.

Kwa upande wake mmoja wa wazee waliopo katika makao hayo, Clement Swalehe, alisema serikali kwa sasa imewatelekeza kwani hata huduma za afya walizokuwa wakizipata hapo awali, kwa sasa hawazipati tena.

“Sasa hivi ukizidiwa hapa wanakupeleka hospitali ya Bukumbi tukifika pale hatupati huduma nzuri tunaishia kuambiwa wanaidai serikali fedha za nyuma” alisema Swalehe.

Naye Anastazia John amemuomba Rais ajae kuwapa kipaumbele hususani cha chakula kwa kuwa sasa wanategemea kutoka kwa baadhi ya watu wanaoguswa japokuwa hakiwatoshi.

“Hii hali ndiyo inasababisha baadhi ya wenzetu kutoka kambini na kwenda mjini kuombaomba misaada barabarani kitendo kinachochangia sisi tunaobaki huku kukosa msaada”. alisema Anastazia John.

Kuhusu taarifa zetu za www.dkmandai.com au matangazo piga simu namba 0716 300 200, 0754 391 743, 0784 300 300. Barua pepe, dkmandaitz@gmail. Au fika ofisini kwetu Ukonga, Mongolandege jijini Dar es Salaam.

No comments:

Post a Comment