Monday, 8 June 2015

VITA VYA KWANZA VYA DUNIA KUKUMBUKWA JUNI 10 DAR


Wizara ya Maliasili na Utalii kupitia Ofisi ya Makumbusho ya Taifa kwa kushirikiana na Ubalozi wa Ubelgiji kwa pamoja wameungana na kuandaa maadhimisho ya kukumbuka vita ya kwanza ya dunia.

Akizungumza katika mkutano na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam Balozi wa Ubelgiji nchini Tanzania, Koen Adam amesema kuwa historia ya vita hivyo imeonekana kutofahamika vizuri miongoni mwa watu wengi nchini Ubelgini na hapa Tanzania pia.

Balozi wa Ubelgiji nchini Tanzania, Koen Adam alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari (hawapo pichani) jijini Dar es Salaam


Balozi huyo aliendelea kusema kuwa katika vita hivyo maelfu ya askari walipoteza maisha yao, lakini ni watu wachache sana ambao wanafahamu ukubwa wa vita hivyo. Hivyo Ubelgiji inataka kuchangia katika kuziba pengo hilo la kumbukumbu na kuleta faida katika maadhimisho hayo ambayo yatahusisha maonesho ya picha 71 na video tatu fupi zinazozungumzia vizuri historia hiyo.

Naye Mkurugenzi Mkuu wa Makumbusho ya Taifa, Prof Audax Mabulla amesema kuwa, onesho hilio litafunguliwa rasmi Juni, 10, 2015 na Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe; Lazaro Nyalandu na siku hiyo hakutakuwa na kiingilio chochote.
Mkurugenzi Mkuu wa Makumbusho ya Taifa, Prof Audax Mabulla akizungumza na waandishi wa habari (hawapo pichani) jijini Dar es Salaam
Pamoja na hayo, Prof. Mabulla amesema maonesho hayo yatadumu hadi Julai 10, 2015, huku yakihusiha mdahalo wa wazi ulioandaliwa kwa kushirikiana na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam juu ya historia hiyo.

Prof. Mabulla pia amewasihi watanzania wote kwa ujumla kufika siku hiyo katika maonesho hayo hususani wanafunzi wa shule za sekondari pamoja na vyuo ili kujifunza mambo mengi kuhusu historia ya vita vya kwanza vya dunia.
Bwana Lucas Catherine huyu ni mwana historia wa Kibelgiji ambaye alianzisha maonesho haya

Miongoni mwa washiriki na waandaaji katika maonesho hayo
Moja ya picha yenye kuonesha historia ya vita hivyo vya kwanza vya dunia
Hata hivyo, Prof Mabulla aliwataka watanzania kutambua thamani ya Makumbusho ya Taifa na kutembelea pale wanapopata nafasi. Ambapo alisema kuwa " watu wako radhi siku za sikukuu waende bichi au bar, lakini si Makumbusho ya Taifa wakati hii ni sehemu muhimu ya kujifunza kuanzia kisayansi, kiutamaduni na kihistoria".

Mbali na hayo Prof Audax Mabulla amesema kuwa ofisi yake imepokea  kwa heshima kubwa kwa kushirikia kuandaa onesho hilo la kipekee lenye lengo la kuelezea historia baina yetu Tanzania, Ubelgiji na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo kuhusu vita hiyo.

Asante kwa kuendelea kuwa karibu na tovuti yetu na kuifanya kuwa mahali pakupata taarifa mbalimbali. Tambua kuwa tunatambua thamani yako na tunaomba endelea kuwa nasi kila siku

No comments:

Post a Comment