Thursday, 25 June 2015

WAKATI WASAKA URAIS WENGINE WAKITUMIA MAGARI MAZURI NA HATA NDEGE KUZUNGUKA MIKOANI, YULE MGOMBEA MKULIMA YEYE ANATUMIA USAFIRI HUU!!!


Wakati wagombea mbalimbali kupitia Chama cha Mapinduzi CCM wakizunguka mikoani kutafuta wadhamini naye kada wa chama hicho Elidephonce Bilohe (43) ambaye ni mkulima ameendelea kufanya hivyo lakini kwa aina yake.

Bilohe ambaye anaomba kupitishwa na chama chake kuwania urais, amesema yeye anatumia usafiri wa mabasi ya umma kuzunguka mikoani kusaka wadhamini.

Sasa wakati Bilohe akitumia usafiri huo, wagombea wenzake wao wameendelea kuonekana wakitumia mabasi yakukodi ambayo wamekuwa wakiyafanyia maboresho ndani, magari madogo na wengine wamekuwa wakitumia ndege kutafuta wadhamini 450 kutoka mikoa 15 inayotakiwa kwa mujibu wa taratibu za CCM.

Bilole amesema hadi sasa ameshafika mikoa tisa ambayo ni Dodoma, Geita, Mwanza, Simiyu, Shinyanga, Kigoma, Tabora, Morogoro na Dar es Salaam, tangu alipochukua fomu hiyo Juni 9.

“Huko kote nimekuwa nikienda kwa kutumia usafiri wa mabasi ya abiria na daladala. Kwa kweli nimepata ushirikiano mzuri kutoka kwa makatibu wa CCM, nawashukuru sana,” alisema Bilole.

Hata hivyo, Bihole amesema huwa anatumia siku mbili ama tatu kufika mkoa mmoja, huku akidai kutumia gharama nyingi katika zoezi hilo.

“Kwenda mkoa mmoja natumia siku mbili ama tatu kufika na kupata wadhamini. Gharama ni nyingi sana, lakini kwa kuwa nimeshaamua kuwatumikia Watanzania nitakwenda,” alisema.

Aidha, Bilohe alisema atakwenda mikoa 15 tu kama inavyohitajika na chama chake, tofauti na watiania wengine ambao baadhi wamekwenda zaidi ya mikoa 20.

Mbali na hayo, amesema kuwa Watanzania wamekuwa wakimtia matumaini katika safari yake hiyo na kuwaomba wamuombee ili aweze kuifanikisha kwa mafanikio.

“Naomba Watanzania wenzangu mniombee katika safari hii. Nitawavusha kuwapeleka kwenye nchi ya ahadi,” alisema Bilohe aliyejiunga na chama hicho mwaka 2003.

Bilohe ni mmoja wa makada wachache waliojitokeza kuomba ridhaa ya CCM ambao hawajawahi kushika madaraka makubwa serikalini au ya kisiasa.

Hadi sasa jumla ya makada 39 wamejitokeza kuwania nafasi hiyo na Bilohe ndiye mgombea pekee aliye na elimu ndogo ya darasa la saba, tofauti na sheria ya nchi inayotaka mgombea wa nafasi hiyo ya juu kisiasa awe na shahada.

CHANZO: MWANANCHI

 Unaweza kuwasiliana nasi kwa maelezo zaidi au ushauri, piga simu namba 0716 300 200, 0754 391 743, 0784 300 300. Barua pepe, dkmandaitz@gmail. Au fika ofisini kwetu Ukonga, Mongolandege jijini Dar es Salaam.

No comments:

Post a Comment