Thursday, 16 July 2015

MATOKEO KIDATO CHA SITA, ZIFAHAMU SHULE KUMI BORA NA ZILE ZILIZOFANYA VIBAYA


Imeelezwa kuwa ufaulu wa kidato cha sita umeongezeka baada ya watahiniwa 38,853 kati ya watahiniwa 40,753 waliofanya mtihani wa Kidato cha Sita kwa mwaka 2015 kufaulu ikiwa ni ongezeko la asilimia 1.67 ukilinganisha na matokeo ya mwaka jana.

Hayo yamesemwa na Katibu Mtendaji wa Baraza la Mitihani Tanzania (Necta), Dk Charles Msonde wakati akitangaza matokeo hayo, ambapo alisema watahiniwa waliofaulu ni asilimia 97.65 ukilinganisha na watahiniwa 38,905 ambao ni asilimia 95.98 wa mwaka jana.

Aidha, katika matokeo hayo watahiniwa waliofaulu, wasichana ni 11,737, sawa na asilimia 98.56 wakati wavulana ni 27,119 ambayo ni asilimia 97.27.

Akizungumzia matokeo ya watahiniwa wa shule, Katibu Msonde alisema watahiniwa 34,777 ambao ni sawa na asilimia 98.87 walifaulu mitihani yao ikiwa ni ongezeko la asilimia 0.61.

Wasichana wakiwa ni 10,576 sawa na asilimia 99.46 na wavulana ni 24,201 sawa na asilimia 98.61. Kwa mwaka jana watahiniwa 34,645 ambao ni asilimia 98.26 walifaulu mitihani yao.

Kwa upande wa watahiniwa wa kujitegemea, Msonde alisema watahiniwa 4,076 sawa na asilimia 88.34 wamefaulu mitihani yao. Mwaka jana watahiniwa 4,260 ambao ni asilimia 80.73 walifaulu mitihani yao.

Katibu Mtendaji wa Baraza la Mitihani Tanzania (Necta), Dk Charles Msonde akitoa matokeo ya kidato cha sita
Akizungumzia madaraja ya ufaulu, Msonde alisema watahiniwa 31,450 ambao ni asilimia 89.41 wamefaulu katika daraja la juu ya Distiction, Merits na Credit, wasichana wakiwa ni 9,876 na wavulana 21,574.

Aidha, Msonde alisema takwimu za matokeo zinaonesha kuwa ufaulu wa watahiniwa wa shule katika masomo ya Historia, Jiografia, Kiingereza, Fizikia, Kemia na Bayolojia umepanda ukilinganisha na mwaka jana huku ufaulu wa juu ni wa masomo ya Historia na Kiswahili ambao ni asilimia 99.96.

Pia Katibu Msonde aliongeza kuwa ufaulu wa masomo ya sayansi ya Kemia na Fizikia umeimarika ukilinganisha na mwaka jana huku ufaulu wa masomo ya Maarifa, Kilimo, Hisabati ukishuka kidogo.

Pmaoja na hayo Katibu Msonde alizitaja shule 10 bora zilizofanya vizuri, Msonde kuwa ni Feza Boys, Runzewe, Feza Girls, Sumbawanga, Ivumwe, St Marys’ Mazinde Juu, Vwawa, Kisimiri, Namabengo na Scolastica.

Kwa upande wa zile shule 10 zilizofanya vibaya kuwa ni Bariadi, Ilongero, Lwangwa, Kilangalanga, Kaliua, Lugoba, Iwalanje, Mtwara (Ufundi), Kwiro na Meta. “Tathmini inaonesha kwamba shule kumi bora kitaifa, shule tano ni za serikali na tano zisizo za Serikali, katika shule 20 bora kitaifa, shule 13 za Serikali na saba ni zile zisizo za Serikali,” alisema.

Halikadhalika aliwataja wanafunzi waliofanya vizuri katika masomo ya sayansi kuwa ni Rosemary Chengula (St Mary’s Mazinde Juu), Ramadhani Ngembe (Feza Boys), Lesian Lengare (Ilboru), Hunayza Mohamed (Feza Boys), Kevin Rutahoile na (St Joseph Cathedral), Anderton Masanja (St. Joseph Cathedral), Joseph Pasian (Ilboru), Lupyana Kinyamagoha (Mzumbe), Yonazi Senkondo (Feza Boys), Meghna Solanki (Shaaban Robert).

No comments:

Post a Comment