Monday, 3 August 2015

CHADEMA YAANZA VIKAO VYAO JIJINI DSM

Kikao cha Sekretarieti ya Kamati Kuu ya Chama cha Demokraria na Maendeleo(Chadema), kimeanza rasmi jana huku Naibu Katibu Mkuu wake upande wa Bara John Mnyika akiibuka kwenye kikao hicho.

Mnyika kwa siku kadhaa alikuwa hajaonekana tangu Waziri Mkuu wa zamani Edward Lowassa aliyekuwa kada wa CCM kujiunga na Chadema.

Kutoonekana kwa Mnyika wakati wa kumpokea Lowassa kuliibua maswali mengi lakini kuhudhuria kwake kikao cha jana kimerudisha matumaini mapya kwa waliokuwa na hofu dhidi yake.

Hata hivyo, Katibu Mkuu wa Chadema Dk.Wilbrod Slaa yeye hajaonekana kwenye kikao hicho huku kukiwa hakuna taarifa zozote za kutofika kwake.

Dk.Slaa tangu Lowassa kuhamia Chadema hajaonekana hadharani hali inayosababisha maswali mbalimbali huku wengine wakidai amechukizwa na ujio wa kada mpya ndani ya chama hicho.

Kikao kilichoanza jana ni kwa mujibu wa ratiba ya Chadema ya kuanza kwa vikao vya ngazi ya juu vyenye lengo la kujadili masuala muhimu kuelekea uchaguzi mkuu unaotarajia kufanyika Oktoba 25 mwaka huu.

Pamoja na kuanza kwa kikao hicho katika Hoteli ya Bahari Beach Dar es Salaam , waandishi wa habari hawakuruhusiwa kuhudhuria kikao hicho.Hata hivyo taarifa zinaeleza kuwa kikao hicho lengo lake ni kuweka mikakati mbalimbali ya namna ya kufanikisha ushindi katika uchaguzi mkuu na mambo mengine yanayohusu chama hicho.

Pia imefahamika kuwa kikao hicho kitajadili kutoonekana kwa Dk.Slaa na huenda leo hii chama kikatoa tamko rasmi ili umma wa Watanzania ufahamu.

Mwenyekiti wa Chadema Freeman Mbowe juzi alitoa ratiba ya vikao katika chama hicho ambapo jana vilianza vikao vya kamati kuu.

Wakati leo kutakuwa na kikao cha mkutano wa Baraza Kuu na kesho hadi Agosti 8 mwaka huu kutakuwa na mkutano mkuu utapitisha jina la mgombea urais na mgombea mwenza na kutangaza ilani ya chama itakayotumika katika uchaguzi.

Pia, Agosti 5 hadi 8 mwaka huu, Kamati Kuu itakaa kuchagua wabunge na kazi kubwa ya Ukawa ni kuzalisha viongozi wenye sifa za kuongoza nchi.

Source: Jambo Leo

No comments:

Post a Comment