Tuesday, 18 August 2015

DAR YAKUMBWA NA KIPINDUPINDU, ZIPO HAPA DALILI ZA UGONJWA HUO NA NAMNA UNAVYOWEZA KUENEA

Ugonjwa wa kipindupindu  umeingia Dar es Salaam na kusababisha watu wawili kupoteza maisha na wengine 26 kulazwa katika hospitali ya Mwananyamala na Sinza.

Hayo yamebainishwa na Mkurugenzi Mtendaji wa Manispaa ya Kinondoni, Mhandisi Musa Nati, ambaye alisema watu wengine wanne wamethibitika kuugua ugonjwa huo na waliolazwa katika hospitali hizo wameonekana kuwa na dalili za ugonjwa huo.

Nati alisema kuna wodi mbili ambazo zimetengwa katika hospitali hizo kwa ajili ya wagonjwa wenye dalili hizo.

Aidha, Mkurugenzi huyo amearifu kuwa kwa sasa wanaandaa kambi maalum kwa ajili ya wagonjwa wa kipindupindu katika eneo la Mburahati, huku akibainisha kwamba wameanza kuchukua tahadhari kwa kupuliza dawa katika maeneo yaliyoripotiwa kuwa na mlipuko wa ugonjwa huo.

"Maeneo tuliyopuliza dawa ni Manzese, Tandale na vitongoji vya Kijitonyama katika Wilaya ya Kinondoni"  alisema Nati.

Hapo awali Mganga Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, Aziz Msuya alisema mmoja wa wagonjwa alifariki dunia wakati akipelekwa hospitali ya Mwananyamala na mwingine wa pili alifariki  akiwa nyumbani na mwili wake kupelekwa Hospitali ya Sinza kuhifadhiwa.

Dk Msuya pia aliwasihi wananchi kuchukua tahadhari pale wanapoona mgonjwa anakuwa na dalili za ugonjwa huo na wamuwaishe katika kituo cha afya, lakini pia amewataka wananchi kunawa mikono kila wakati wanapotoka msalani au kusalimiana na watu kwa kushikana mikono.

Naye Mganga Mkuu wa Hospitali ya Mwananyamala, Sophinias Ngonyani alisema wagonjwa waliothibitika kuwa na kipindupindu ni wawili na wengine kumi na moja bado sampuli zao ziko maabara

Dondoo Muhimu Kuhusu ugonjwa huu:
Ni vyema aikafahamika kwamba kipindupindu ni ugonjwa ambao husababishwa na aina ya bakteria waitwao vibrio cholerae.

Ugonjwa huu huambukizwa kwa njia ya viini vinavyoenezwa kupitia kinyesi kutoka kwa mgonjwa mwenye kipindupindu kwenda kwa mwingine.

Dalili za ugonjwa huu ni kutapika, kuharisha na kupungukiwa na maji mwilini na endapo mgonjwa hatapata tiba ya mapema basi huweza kupoteza maisha.

Usisite kutangaza biashara yako au taarifa yako yoyote kupitia tovuti hii ili uwafikie watu wengi kwa wakati mmoja. gharama zetu ni nafuu sana wasiliana nasi sasa kwa simu namba 0784 300 300, 0769 400 800, 0716 300 200 au barua pepe dkmandaitz@gmail.com


No comments:

Post a Comment