Friday, 7 August 2015

HAYA NDIYO MAAJABU YA MUAROBAINI KATIKA TIBA

Mwarobaini ni mti maarufu sana na unajulikana karibu kila mahali , huku ukielezwa kuwa mti huo ni kati ya miti mirefu yenye ukijani mzuri sana, ingawaje majani yake ni machungu mno.

Mti huo umekuwa ukifahamika kwa uwezo wake wa kutibu magonjwa ya aina mbalimbali, huku ikiaminika kwamba mti huo asili yake ni nchini India. Pia mwarobaini hustawi zaidi katika nchi za tropiki na una uwezo mkubwa wa kuhimili hali ya ukame.

Kwa hapa nchini, mti wa mwarobaini huweza kupatikana kwa urahisi kabisa katika maeneo mengi ya mijini na vijijini pia.

Jina la mti huu ‘mwarobaini’ linatokana na imani kuwa mti huu una uwezo wa kutibu magonjwa yapatayo arobaini, huku majani yake na mbegu zikitumiwa kama tiba kwa miaka.

Mtaalam wa tiba asili hapa jijini Dar es Salaam Dk Abdallah Mandai, anasema kwamba magome ya mti wa mwarobaini yakichemshwa huwa ni dawa ya kuua minyoo yote tumboni, homa, kikohozi na kujisikia kuwaka moto, kuharisha pamoja na tatizo la vidonda vya tumbo, n.k

Aidha, mtaalam huyo anasema kuwa majani ya mti huo yanapowekwa katika maji moto huweza kutibu matatizo ya macho, maumivu ya ini pamoja na magonjwa ya ngozi.

Pamoja na hayo, Dk Mandai anabainisha kuwa matunda ya mti wa mwarobaini pia yanaelezwa kusaidia matatizo ya matezi, bawasira pamoja na matatizo ya meno, huku akiongeza kuwa mti huo pia umekuwa ukisaidia katika kutibu magonjwa mbalimbali ya ngozi.

No comments:

Post a Comment