Monday, 24 August 2015

HIZI NDIZO AHADI ZA MAGUFULI KWA WATANZANIA


Mgombea urais kwa tiketi ya Chama cha Mapinduzi CCM, Dk John Magufuli  jana alifungua rasmi kampeni za chama hicho kwenye viwanja vya Jangwani jijini Dar es Salaam mkutano ambao ulihudhuriwa na maelfu ya wananchi, huku akitaja vipaumbele vyake muhimu endapo atachaguliwa kuwa rais.

Magufuli aliahidi kuanzisha mahakama maalum ya kusikiliza kesi za rushwa na ufisadi, kumaliza tatizo la mikopo kwa wanafunzi wa elimu ya juu, kuulinda muungano na usalama wa nchi pamoja na kuhakikisha anatetea haki za wasanii na mama lishe kuachwa kubugudhiwa.

Ahadi nyingine ni kusimamia nishati ya gesi, ujenzi wa barabara, reli, kuboresha sekta ya utalii, kuimarisha uwekezaji, kuwasaidia walemavu na kusimamia uhuru wa habari.

Magufuli pia aliahidi kutoingilia utendaji kazi wa mahakama na bunge, kuheshimu mawazo ya vyama vingine,  kuimarisha vyombo vya ulinzi na uasalama, kuendeleza kilimo, mifugo, uchimbaji wa madini, maji safi na elimu bora sambamba na kuhakikisha wafanyabiashara wadogo na wakubwa wote wanalipa kodi.

Pamoja na hayo, pia ameahidi ajira kwa watanzania ambapo alisema "nina taka Watanzania wapate ajia, kazi ya serikaliitakuwa kukusanya kodi tu, viwanda vinaweza kutengeneza ajira kwa asilimia 40 hasa kwa vijana wanaohitimu vyuo mbalimbali"

Kuhusu afya Mgufuli  alisema "tutahakikisha tunakuwa na vituo vya afya, zahanati na hospitali katika maeneo mbalimblai kwa sababu tunaamini maendeleo ya kweli hayawezi kupatikana kama wananchi hawana afya bora" 

Pia aliendelea kuahidi kuwa "mishahara ya walimu na wafanyakazi wote tutaishughulikia pamoja na madereva haki zao za msingi lazima ziangaliwe'

Hata hivyo, Magufuli alisema kuwa mabadiliko ya kweli hayawezi kupatikana endapo kutakuwa na matabaka miongoni mwa Watanzania.

"Tutahakikisha tunakuwa na umoja wa kitafa, lazima watu wote wawe wamoja hakuna ukabila, udini nimejiandaa kulinda umoja wa Watanzania wote"

No comments:

Post a Comment