Wednesday, 19 August 2015

IDADI YA WALIOFARIKI KWA UGONJWA WA KIPINDUPINDU YAONGEZEKA DAR, SABABU YA VIFO YATAJWA


Wauguzi katika kambi ya wagonjwa wa kipindupindu iliyopo hospitali ya Mwananyamala, Dar es Salaam wakiwa kwenye eneo lao la kazi jana.
Mwanzoni mwa wiki hii ndipo zilipoanza kuripotiwa taaarifa za mlipuko wa ugonjwa wa kipindupindu, huku watu wawili wakiripotiwa kupoteza maisha kutokana na ugonjwa huo.

Sasa leo taarifa mpya ambayo si nzuri pia ni kwamba kuna watu wengine watatu wamethibitika kufa kwa ugonjwa wa kipindupindu jijini Dar es Salaam na  hivyo kufanya waliokufa kwa ugonjwa huo kufikia watano, huku wagonjwa waliolazwa katika hospitali mbalimbali za wilaya ya Kinondoni wakifika 34.

Akitoa taarifa hiyo Dar es Salaam jana, Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, Paul Makonda alisema wagonjwa hao wanatoka katika maeneo ya Kijitonyama, Kimara, Manzese, Tandale, Saranga, Makumbusho, Kimara na Mwananyamala.

Makonda alisema hadi kufikia watu watano walikuwa wamekufa, huku 34 wakilazwa, ambapo 18 walikuwa wamelazwa katika Hospitali ya Mwananyamala na wengine 16 katika Hospitali ya Sinza. “Kati ya wagonjwa 18 waliolazwa Mwananyamala, wakubwa ni wanne na watoto 14.

Kati ya 16 waliolazwa Sinza watatu ni wanawake na 13 ni wanaume, vifo ni vitatu,” alisema. Kutokana na ugonjwa huo, Serikali ya Kinondoni imejipanga kukabiliana na ugonjwa huo ikiwemo dawa, vifaa tiba vya kutosha ili kuweza kukabiliana na ugonjwa huo.

“Tumefungua kambi yetu katika zahanati ya Kijitonyama ambayo ina dawa na vifaa tiba vyote vinavyohitajika ili kuhudumia wagonjwa hao ipasavyo,” alisema. Makonda mkuu huyo wa wilaya na kubainisha kwamba wagonjwa wengi ambao wameripoti hospitalini walifika wakiwa wamechelewa hivyo kuwa vigumu kuokoa maisha yao.

Naye Mganga Mkuu wa Manispaa hiyo, Dk Aziz Msuya alisema wagonjwa wote waliokufa walicheleweshwa kufika hospitalini, hivyo kushauri mara mgonjwa anapoona dalili hizo awahi haraka kwenye kituo cha afya. Pia alisema wamehamisha kambi ya wagonjwa waliokuwa Sinza na kuwapeleka kwenye kambi mpya eneo la Mburahati.

Source: Habari Leo

No comments:

Post a Comment