Thursday, 20 August 2015

IFAHAMU HII MIPANGO YA RAIS KIKWETE BAADA YA MUDA WAKE WA URAIS KUMALIZIKA

Rais Jakaya Kikwete
Rais Jakaya Kikwete ameeleza ndoto yake baada ya muda wake wa urais kumalizika, kuwa ataanzisha taasisi ya maendeleo, itakayosimamia midahalo, semina na kongamano kwa maendeleo ya taifa.

Rais Kikwete Alisema hayo Ikulu, Dar es Salaam jana, alipopokea Shahada ya Heshima kutoka Taasisi ya Sayansi na Teknolojia ya Nelson Mandela.

Rais Kikwete alisisitiza ndoto yake ni kuanzisha taasisi hiyo ya maendeleo, ambayo kazi yake kubwa itakuwa kujadili, kupokea, kutafuta wadhamini na kushauri juu ya masuala yatakayoiletea maendeleo nchi.

Aidha,  alitaja baadhi ya masuala ya maendeleo yakayopewa kipaumbele na taasisi hiyo kuwa ni pamoja na afya, afya ya akinamama na watoto, kilimo, maendeleo ya sayansi na teknolojia na viwanda.

“Kuna watu wamenishauri nianzishe taasisi ya kushughulikia migogoro, sitaki kabisa kuitwa mchawi na wala taasisi hiyo siitaki kabisa, ila mgogoro ukitokea na nikahitajika, basi nitachangia; Ila dhamira yangu ni kushughulikia masuala ya maendeleo, alisema.

Pia Rais Kikwete amesema atakapostaafu ataishi kijijini kwao Msoga, Chalinze mkoani Pwani, kuendeleza ufugaji na kilimo cha nanasi na hatapenda kujishughulisha kwa kiwango kikubwa na masuala ya serikali.

“Kusema ukweli nitakapostaafu sitopenda kujishughulisha sana na masuala ya kiserikali, kwa sababu atakuwepo Rais mwingine lakini pia nitapenda nijishughulishe na shughuli zangu nilime mananasi na kufuga. Ila nitajaribu kuchangia kwa kadri ya uwezo wangu,” alisisitiza Rais Kikwete

Source: Habari Leo

No comments:

Post a Comment