Friday, 21 August 2015

JAJI MUTUNGIA AVITAKA VYAMA VYA SIASA KUFANYA KAMPENI ZA KISTAARABU

Ikiwa upepe wa siasa sasa karibu unaanza kuelekea kwenye kampeni, msajili wa Vyama vya Siasa nchini, Jaji Francis Mutungi ameviagiza vyama vya siasa kudhibiti vitendo vya wanachama wake vinavyoweza kusababisha uvunjifu wa amani.

Jaji Mutungi amesema kuna baadhi ya wanachama na mashabiki wa vyama huwazomea na hata kuwarushia mawe wanachama na mashabiki wa vyama vingine, hasa pale wanapovaa sare za vyama vyao.

Jaji Mutungi katika taarifa yake kwa umma amevitaka na kuviagiza vyama vyote vya siasa, kutoa maelekezo kwa wanachama wake wote na kuwataka wawe na utulivu katika kipindi chote cha Uchaguzi kwa kuheshimu sheria na kuzingatia dhana ya kufanya siasa za kistaarabu ikijumuisha kuwa na uvumilivu wa kisiasa.

“Siku za hivi karibuni kumejitokeza tabia ya baadhi ya wanachama na mashabiki wa baadhi ya vyama vya siasa kuwazomea na hata kuwarushia mawe wanachama na mashabiki wa vyama vingine na hasa pale wanapovaa sare za vyama vyao,” alisema Jaji Mutungi.

Jaji Mutungi alisema katika kipindi cha uchaguzi ni kipindi ambacho kuna ushindani mkubwa na matukio mengi ya kisiasa, hali ambayo inahitaji vyama vya siasa kuzingatia sana utii wa sheria za nchi na kufanya siasa za kistaarabu, ili kujiepusha na vitendo/matendo yanayoashiria uvunjifu wa amani.

Aidha, ameviagiza vyama vyote vya siasa kutoa maelekezo kwa wanachama wake wote na kuwataka wawe na utulivu katika kipindi chote cha uchaguzi na kuheshimu sheria na kuzingatia dhana ya kufanya siasa za kistaarabu na utulivu.

Kauli ya Jaji Mutungi imekuja huku Polisi wa Kanda ya Dar es Salaam wakitoa onyo kwa watu wanaojihusisha na vitendo vya kuzomea waliovalia sare za vyama na kusema hatua za kisheria zitachukuliwa dhidi yao.

No comments:

Post a Comment