Saturday, 22 August 2015

JESHI LA POLISI: VIKUNDI VYA ULINZI VYA VYAMA NI MARUFUKU

Polisi nchini imepiga marufuku vikundi vya ulinzi vya vyama vya kisiasa , vyenye mwelekeo wa kijeshi kufanya kazi za ulinzi hadharani kwa madai kuwa vinaingilia majukumu yao.

Onyo hilo lilitolewa jana na Kamishna wa Polisi–Operesheni na Mfunzo, Paul Chagonja wakati akizungumza na waaandishi wa habari Makao Makuu ya Polisi, Dar es Salaam.

Chagonja alivitaja vikundi hivyo na vyama vyao kuwa ni Green Guard (CCM), Red Brigade (Chadema) na Blue Guard (CUF), ambavyo hutumiwa na vyama vya siasa hususani katika mikutano yao.

Agizo la Chagonja limekuja ikiwa ni miezi minne baada ya agizo la Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini, Inspekta Jenerali wa Polisi (IGP), Ernest Mangu kupiga marufuku vikundi hivyo vya vyama vya siasa ambavyo vina muonekano na muundo wa vyombo vya usalama, kwani ni kinyume cha katiba na sheria ya nchi.

Alivitaka vyama hivyo kuhakikisha vinafuata muongozo uliotolewa na Ofisi ya Msajili wa vyama hivyo na kama vikienda kinyume jeshi litapambana navyo.

No comments:

Post a Comment