Tuesday, 25 August 2015

KAMPENI ZASHIKA KASI SASA LOWASSA AONJA JOTO LA USAFIRI WA DALADALA, ASEMA LENGO LAKE NI KUTAKA KUJUA KERO ZA USAFIRI HUO

Mgombea urais kwa tiketi ya Chadema, Edward Lowassa (kushoto) akilipa nauli kwa kondakta wa daladala iliyokuwa ikitoka Gongo la Mboto kuelekea Chanika
Ikiwa ni siku tatu sasa tangu kuanza kwa kampeni na huu ndio ule wakati wa kila mgombea kutumia ubunifu, akili na utashi zaidi ili kuhakikisha anawafikia wananchi na kueleza dhamira yake ya kuhitaji uongozi.

Kwa upande wa Chama cha Mapinduzi CCM wao walianza juzi Agosti 23, 2015 katika viwanja vya Jangawani jijini Dar es Salaam, lakini jana Agosti 24 mgombea urais kwa tiketi ya CHADEMA Edward Lowassa naye alinza rasmi kampeni zake ndani ya jiji hilo kwa staili yake ya kipekee.

Lowassa aliamua kusafiri kwa kutumia daladala ili kuangalia hali ya usafiri wa umma ambapo aliwasili asubuhi saa 1:51 akiwa katika msafara wa magari matano, huku akiambatana na mgombea mwenza Juma Duni Haji, Msemaji wa Jumuiya na Taasisi ya Kiislam, Sheikh Rajabu Katimba pamoja na walinzi wake.
Baada ya kuwasili mgombea huyo alishuka kwenye gari alilokuwa amekuja nalo na kuanza kuzungumza na abiria na wafanyabiashara waliokuwa kituoni hapo.

Ilipofika saa mbili kama na nusu hivi Lowassa aliamua kuingia kwenye daladala moja iliyofika kituoni hapo kupakia abiria naye akapanda na kusafiri nayo hadi Chanika, lakini baadhi ya abiria walitahamaki kumuona Lowassa akiingia kwenye daladala hiyo na badhi yao waliteremka kwa mshangao.
Ndani ya daladala hiyo Lowassa alikuwa amekaa kiti kimoja na mwanafunzi na ulipofika muda wa kulipa nauli kondakta alisema "Kwa kuwa wewe ni rais mtarajiwa sita kutoza nauli, utapanda bure"ombi ambalo Lowassa alikataa na kutoa noti ya shilingi 2,000 na kumtaka konda achukue nauli yake pia akate na nauli ya mwanafunzi aliyekuwa amekaa naye. Hata hivyo kondakta alichukua fedha hizo na hakurejesha chenji ya shilingi 1,400 wala kudaiwa.
Mgombea huyo alizungumza na wananchi wa eneo la Chanika na kuawasikiliza kisha kuendelea na ziara yake kuelekea Mbagala kwa kutumia gari lake.

No comments:

Post a Comment