Monday, 10 August 2015

LOWASSA AITUHUMU CCM KWA KUIBA KURA, JAJI LUBUVA AMTAKA KUELEZA JINSI WANAVYOIBA KURA HIZO

Agosti 09, 2015 mgombea urais kupitia CHADEMA, Edward Lowassa alifika katika ofisi za makao makuu ya CUF yaliyopo Buguruni jijini Dar es Salaam na moja ya mambo aliyoyasema jana akiwa katika makao makuu ya chama hicho ni pamoja na kukituhumu chama cha CCM kuwa ni hodari wa kuiba kura.

Kufuatia hali hiyo Lowassa amewataka wananchi kujitokeza kwa wingi na kupiga kura ili hata sehemu ya kura hizo ikiibiwa, Ukawa ishinde kwa kishindo.

Lowassa ambaye ni waziri mkuu wa zamani aliuambia umati wa wafuasi wa Ukawa kuwa ili kufanikisha ushindi na kuwawezesha kuingia ikulu hawana budi kushikamana, kushawishiana na kupiga kura kwa wingi na kuzilinda Oktoba 25.

“Tukiwa na umoja, tukiwa na mshikamano tutawaondoa Jumapili asubuhi sana. Tutahitaji mshikamano, tatahitaji ushawishi wa kupiga kura tupate angalau asilimia 90 ili wakiiba asilimia 10 tuwasamehe,” alisema Lowassa katika hotuba yake.

Hata hivyo, Lowassa hakuwa na vielelezo wala uthibitisho kuhusu tuhuma hizo dhidi ya chama chake cha zamani.

Akitolea ufafanuzi madai hayo, Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) Jaji mstaafu, Damian Lubuva alisema Lowassa angeeleza jinsi wanavyoiba kura.

“Ili kutoa majibu ya uhakika naomba tufanye utafiti wa kutosha juu ya tuhuma hizo, lazima tujue ni njia zipi watu wanaiba, vinginevyo nitaeleza kitu ambacho sina ufahamu nacho. Yeye (Lowassa) kama mtu aliyekuwa serikalini lazima ana ufahamu walikuwa wanaiba vipi, angeeleza.”  alisema Jaji Lubuva.

Katika hatua nyingine Jaji Lubuva amesema kuwa tume huwa inaendesha uchaguzi kwa mujibu wa taratibu na sheria na iwapo kuna mtu anasema kura zinaibwa ajitokeze aeleze kinagaubaga ili ofisi yake ifanye utafiti wa kina.

“Naomba nieleweshwe kura huwa zinaibiwa vipi? Hii imekuwa ni hisia, wengine wanasema tutaibiwa kura zetu wakati upande mwingine unasema hawa wataleta fujo kwa visingizio vya kuibiwa kura,” alisema Jaji Lubuva.

Kama ungependa kutangaza biashara yako na tovuti hii basi wasiliana nasi kwa simu namba 0716 300 200, 0784 300 300, 0769 400 800 barua pepe dkmandaitz@gmail.con

No comments:

Post a Comment