Saturday, 1 August 2015

NEC YATOA RATIBA YA KUCHUKUA FOMU ZA URAIS, YAPIGA MARUFUKU MATAMSHI YA UCHOCHEZI


Tume ya Uchaguzi (Nec) imetangaza kuanzia leo, wagombea wa nafasi ya urais wataanza kuchukua fomu za kuwania kiti hicho zoezi ambalo litadumu hadi Agosti 21, mwaka huu.

Akitangaza ratiba hiyo Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi Damian Lubuva amesema vyama vitatu vya United Peoples Democratic Party (UPDP), Tanzania Labour Party (TLP) na Democratic Party (DP) ndivyo vitaanza kufungua zoezi hilo.

“Tunaanza kutoa Fomu kwa wale wanaogombea urais, kesho (leo) UPDP watakuja kuchukua fomu saa tatu asubuhi wamesema hawana shamrashamra… TLP wao watakuja saa sita mchana wanakuja kwa shangwe… DP wao wanakuja saa nane mchana pia nao wamesema watakuja kwa shangwe pia" alisema Jaji Lubuva

Akiendelea kutoa ratiba hiyo Lubuva amesema “Jumanne August 4 watakuja CCM saa sita mchana watakuja kwa shangwe kama wengine na Jumatano watakuja ADC saa tatu asubuhi, wao hakuna shamrashamra baada ya hapo watakuja TADEA saa nne asubuhi pia wao hawana shangwe”
“August 17 watakuja ACT- Wazalendo saa tatu asubuhi wanakuja kwa shange pia… muda wa kuandisha wapigakura kwa mfumo wa BVR unaisha rasmi August 8 2015 na baada ya hapo ratiba ya tume itaendelea kuruhusu uchaguzi Mkuu” alisema Jaji Damian Lubuva, Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi.

Pamoja na hayo Lubuva amevitaka vyama ambavyo vitakuja na wanachama wao kuchukua fomu hizo (shamrashamra) wahakikishe wanalinda amani ya wananchi.

“Shamra shamra ziwepo lakini zisivunje amani ya wananchi, haki hiyo isifanywe kukatiza uhuru wa watu wengine,” alisema Lubuva.

Mbali na hayo, NEC pia imewaonya wanasiasa wanaotoa matamshi yenye uchochezi, huku akitolea mfano maneno yaliyotamkwa na kiongozi mmoja wa chama cha siasa kuwa chama chake kitashinda Uchaguzi Mkuu ujao hata kwa goli la mkono.

“Viongozi wawe makini wasitoe matamshi yanayoweza kuleta tafsiri mbaya. Goli la mkono ni matamshi yasiyo na breki,” amesema Jaji Lubuva.

No comments:

Post a Comment