Monday, 10 August 2015

PROFESA LIPUMBA: KUMSIMAMISHA LOWASSA KUWANIA URAIS NI SAWA SAWA NA CCM KUSIMAMISHA WAGOMBEA WAWILI WA URAIS

Aliyekuwa Mwenyekiti wa Chama cha Wananchi (CUF), Profesa Ibrahim Lipumba amesema Chama cha Mapinduzi (CCM), ni sawa kimesimamisha wagombea wawili wanaowania kiti cha urais katika Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 25, mwaka huu.

Profesa Lipumba ameyasema hayo juzi usiku katika mahojiano aliyoyafanya na Azam TV kutoka Kigali alikosema anafanya utafiti, Profesa Lipumba alisema kumpa nafasi waziri mkuu mstaafu, Edward Lowassa kuwania urais kupitia Chadema ndani ya Ukawa, ni sawa na CCM kusimamisha wagombea wawili (Lowassa) na Waziri wa Ujenzi, Dk John Magufuli.

Kauli hiyo inafuatiwa ikiwa ni siku chache mara baada ya kujiuzulu uenyekiti CUF, huku akisema hiyo ni moja ya sababu za kuachia nafasi yake kutokana na uamuzi uliofikiwa na Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) kuhusu mgombea urais.

Itakumbukwa kwamba Profesa Lipumba alijiuzulu wiki iliyopita, huku akisema dhamira yake ilikuwa ikimsuta kwa kuwaingiza ndani ya Ukawa watu kutoka CCM, waliokuwa wanapingana na maoni ya wananchi kuhusu rasimu ya Katiba ya Jaji Warioba na kuwapa fursa ya kuwania urais.

Mbali na hayo, katika mahojiano hayo ya simu, Profesa Lipumba amesema swala la yeye kujiuzulu kwake hakutumiwa na CCM kuparaganyisha UKAWA, bali walikuwa tayari wameparaganyika.
 
“Ukweli ni kwamba tumejiparaganyisha wenyewe ndani ya Ukawa. Kwa hiyo Watanzania watakuwa na wanaCCM wawili wanaogombea urais wakati UKAWA tulikuwa na wagombea watatu... mimi, Dk Willibrod Slaa, (Katibu Mkuu wa Chadema) pamoja na Dk George Kahangwa (NCCR-Mageuzi) ambaye alikiri kuwapo makubaliano hayo.
 
“Tulikutana nyumbani kwangu tukakubaliana Dk Slaa apeperushe bendera ya Ukawa, lakini tumewekwa kando,” alisema Profesa Lipumba.

Kama ungependa kutangaza biashara yako na tovuti hii basi wasiliana nasi kwa simu namba 0716 300 200, 0784 300 300, 0769 400 800 barua pepe dkmandaitz@gmail.con

No comments:

Post a Comment