Monday, 24 August 2015

SERIKALI YAWAONYA WATAALAM WA TIBA ASILI AMBAO HAWAJASAJILIWA


Serikali imewataka waganga wa tiba asili kuhakikisha wanajisajili Baraza la Tiba Asili na Tiba Mbadala na kujiepusha na matangazo yanayokizana na taarifa za kiutafiti.

Hayo yamesemwa jana na Mganga Mkuu wa Serikali, Dkt. Margaret E. Mhando kupitia hotuba yake ya ufunguzi wa maadhimisho ya siku ya tiba ya asili ya Mwafrika iliyofanyika katika viwanja vya mnazi mmoja jijini Dar es Salaam.

Mhando alisema kuwa hadi sasa kunawatoa huduma wa Tiba Asili wengi, zaidi ya 75,000 lakini waliokwisha sajiliwa ni 8,168 tu. na hivyo kuwataka ambao bado hawajasajiliwa kufanya utaratibu wa kujisajili kwani kutoa huduma bila kusajiliwa ni koso kisheria.

"Napenda kuchukua nafasi hii kuwakumbusha tena Waganga wa Tiba Asili wote nchini msajiliwe". alisema Mhando.
 

Mhando pia amewataka wataalam wa tiba asili kuepuka matangazo yanayokizanza na taarifa za kiutafiti katika suala zima la kutibu na kuponya magonjwa mbalimbali kwa mfano UKIMWI. Huku akiwataka kushirikiana na wataalamu wa tiba za kisasa katika kupata ufahamu na uelewa mkubwa kuhusu magonjwa na namna ya kutumia dawa mbalimbali ikiwa pamoja na dawa za asili.

Aidha, Mhando amewasihi wataalam wa tiba asili kujiepusha na migongano katika jamii kwa kuepuka kuhusisha ushirikina na uchawi kama chanzo cha ugonjwa.

"Kuna taarifa na migongano mingi ya kutisha juu ya hili la kuhusisha tiba na ushirikina na uchawi na itakuwa jambo la busara kwa waganga wa tiba asili kupitia kwenye SHIRIKISHO LA VYAMA VYA TIBA ASILI kupanga mikakati ya kudhibiti na kuondoa kabisa vitendo vibaya vinavyochafua taaluma hiyo."


Wataalam wa tiba asili wakiwa katika picha ya pamoja na Mganga Mkuu wa Serikali Dkt Margaret E. Mhando kutoka kushoto wapili ni Tabibu Abdallah Mandai hii ilikuwa baada ya mkutano huo
 
Pamoja na hayo, Muhando alisema maadhimisho hayo yamelenga kuhimiza uboreshaji wa dawa asili pamoja na utafiti endelevu wa dawa hizo asili ili kurahisisha upatikanaji wa dawa hizo kirahisi zaidi.
 

Mhando pia amewataka wananchi kutambua kuwa Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii inatambua tiba asili kuwa taaluma rasmi.

Maadhimisho ya Siku ya Tiba ya Asili ya Mwafrika kila mwaka huambatana na ujumbe maalum au kauli mbiu. Ujumbe maalum wa mwaka huu ni “Usimamizi wa Watoa huduma za Tiba Asili katika Bara la Afrika” (Regulation of Traditional Health Practitioners in the African Region).

No comments:

Post a Comment