Thursday, 20 August 2015

VIGOGO WA TATU WA WIZARA YA AFYA WAPANDISHWA KIZIMBANI

Maofisa utumishi watatu wa Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii wamepandishwa kizimbani katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam, wakikabiliwa na mashitaka ya matumizi mabaya ya madaraka na kuisababishia serikali hasara ya zaidi ya Sh milioni 3.7.

Washitakiwa ni Anold Shana, Prisca Mangili na Agness Hugo ambao walisomewa mashitaka mbele ya Hakimu Mkazi, Janeth Kaluyenda.

Wakili kutoka Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), Sophia Ghula alidai walitenda makosa hayo katika tarehe tofauti mwaka 2008.

Katika mashitaka yanayomkabili Shana, anadaiwa kati ya Septemba na Desemba 2008 akiwa Ofisa Utumishi alitumia vibaya madaraka yake kwa kutokutoa maelekezo kwa Mhasibu Mkuu wa wizara hiyo, aondoe jina la mfanyakazi aliyestaafu, Rota Mboya katika orodha ya malipo jambo lililosababisha alipwe Sh milioni 1,194,750 .

Mshitakiwa mwingine, Mangili, anadaiwa kati ya Februari na Juni 2008, alitumia madaraka vibaya kwa kutokutoa maelekezo kwa Mhasibu Mkuu wa Wizara, kuondoa jina la mfanyakazi aliyestaafu, Bibi Kanancia katika orodha ya malipo jambo lililosababisha alipwe Sh milioni 1,682,653.52 .

Naye Hugo anadaiwa Aprili, 2008 alitumia madaraka yake vibaya kwa kutokutoa maelekezo kwa mhasibu mkuu wa wizara kuondoa jina la Eidis Mabu, katika orodha ya malipo na kusababisha alipwe Sh 942,593 na hivyo kuisababishia serikali hasara.

Washitakiwa walikana mashitaka. Upelelezi wa kesi hiyo haujakamilika na imepangwa Septemba 23 mwaka huu kwa ajili ya kutajwa. Wapo nje kwa dhamana baada ya kutimiza masharti ya kuwa na wadhamini wawili waliosaini hati ya Sh milioni mbili kila mmoja.

Source: Habari Leo

No comments:

Post a Comment