Thursday, 3 September 2015

BAADHI YA WANACHAMA WA CHADEMA WAANZA KUMPINGA LOWASSA WAANDAMANA WAKIDAI KUMTAKA DK SLAA

Mabomu ya machozi jana yalirindima katika Makao Makuu ya Chadema, Kinondoni jijini Dar es Salaam baada ya baadhi ya wanachama wa chama hicho kupigwa na wenzao kwa kufanya maandamano hadi katika ofisi hizo wakiunga mkono hotuba iliyotolewa na aliyekuwa Katibu Mkuu wao, Dk Willbrod Slaa.

Maandamano hayo yaligeuka kuwa machungu kwa wanachama hao zaidi ya 200, pale walipokumbana na kipigo kutoka kwa wenzao wa Chadema waliokuwa na fimbo katika ofisi hizo hadi pale polisi walipowasili na kutumia mabomu ya machozi kutawanya watu na kuokoa watu waliokuwa wanashikiliwa.

Wananchi hao, wake kwa waume waliandamana kutoka Ubungo, Manzese na Magomeni huku wakiimba kumpongeza Dk Slaa kwa hotuba aliyoitoa Dar es Salaam juzi akielezea kujiuzulu kwake kutokana na chama hicho kumpokea Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa na kumfanya kuwa mgombea wao wa urais.

Baadhi ya maneno ya waandamanaji hao yalisema: “…Slaa kasema kweli, Lowassa hatumtaki, Slaa kasema kweli, Lowassa hatumtaki na pia waliimba “Lowassa hatumtaki, Chadema tunaondoka.”

Wakitumia Barabara ya Morocco kutokea Magomeni Mapipa, waandamanaji hao waliendelea na safari yao huku wakiwa na mabango yenye kaulimbiu kama nyimbo walizokuwa wakiimba; hadi katika Makutano ya Kinondoni Manyanya, na kuendelea na maandamano hadi katika Mtaa wa Ufipa yalipo Makao Makuu ya Chadema. 


Mmoja wa waandamanaji, Zakayo Ngogo akizungumza katika Makao Makuu ya Chadema alisema maandamano hayo yalilenga kufikisha ujumbe.

“Tumekuja kurudisha kadi za chama chetu (Chadema), hotuba ya Dk Slaa imetupa mwanga mpya, hatuwezi kukaa katika chama chenye ukosefu wa maadili na kinachonuka rushwa na ufisadi. Viongozi wetu hawakutueleza ukweli, ukweli tumeupata kutoka kwa Dk Slaa jana (juzi),” alisema Ngogo akizungumza kwa hasira.

Hata hivyo, kijana huyo hakufika mbali katika kutoa maelezo yake baada ya baadhi ya viongozi wa Chadema kutoka ndani ya ofisi hizo na kuanza kuwahoji waandamanaji hao kama wana kadi za Chadema na kuwaagiza kuzikabidhi, hatua iliyowafanya baadhi kuzitoa, lakini mzozo ulizuka baada ya baadhi yao kutokuwa nazo.

Wakati mzozo huo ukiendelea ghafla waliibuka watu wenye bakora ambao walianza kuwacharaza fimbo waandamanaji hao kwa madai kuwa wametumwa na viongozi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) na kwamba hawakuwa wanachama halisi wa Chadema, jambo walilosema haliwezi kuvumilika.

Vurugu hizo ambazo zilisababisha baadhi ya watu kuumia na kukimbizwa hospitali na wengine kuwekwa chini ya ulinzi mkali wa vijana wa Chadema, zilidhibitiwa dakika chache baadaye, baada ya polisi kuwasili katika eneo hilo na kupiga mabomu ya machozi ili kudhibiti vurugu hizo na kuwaokoa mateka.

Akizungumzia tukio hilo Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Kipolisi wa Kinondoni Camilius Wambura, alithibitisha kutokea kwa tukio hilo na kusema vijana hao hawakufuata taratibu za kuandaa na kushiriki maandamano na hivyo maandamano yao yalikuwa batili.


Source: Habari Leo

No comments:

Post a Comment