Advertisement

Advertisement

.

.

Mixer

Mixer

Friday, 18 September 2015

FAHAMU KUHUSU HAYA MANENO YA JAMES MBATIA YALIYOIFANYA SERIKALI KUSIKITISHWA

http://3.bp.blogspot.com/-bz4SHgrXJLE/Vda0LY7N08I/AAAAAAAAGq4/1B_KQjdiLn4/s1600/Jame%2BMbatia.jpgSerikali imeelezea kusikitishwa na taarifa za vyombo vya habari, zinavyomnukuu mmoja wa viongozi wa vyama vya upinzani vilivyounda Ukawa, akidai safari za nje za Rais Jakaya Kikwete ni za ufujaji fedha.

Kiongozi huyo wa Ukawa, James Mbatia Jumanne usiku wiki hii akiwa katika mkutano wake na vyombo vya habari uliorushwa moja kwa moja na vituo vya televisheni na redio, alidai katika kipindi cha utawala wake, Rais Kikwete ametumia zaidi ya Sh trilioni nne katika safari 409, fedha ambazo ni nyingi na zingeweza kutumika kwa shughuli za maendeleo.

Lakini, Serikali kupitia Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali kwa Umma cha Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, ilifafanua katika taarifa kwa vyombo vya habari, jana, kuwa tangu Rais Kikwete aingie madarakani mwaka 2005, kiasi kikubwa cha bajeti kuwahi kutengwa kwa ajili ya safari za Viongozi Wakuu yaani Rais, Makamu wa Rais na Waziri Mkuu ni Sh bilioni 50.

Ilisema kiasi hicho kilitengwa katika mwaka wa Fedha 2014/2015 kwa ajili ya Idara ya Itifaki na kwamba kwa miaka mingine yote, wastani umekuwa ni kati ya Sh bilioni tano hadi 25 kulingana na mahitaji ya idara hiyo.

Katika ufafanuzi huo, ilisema kiasi hicho cha Sh bilioni 50 ni bajeti nzima ya Idara ya Itifaki, ambapo kuna fungu maalumu kwa ajili ya ziara za viongozi.

Ilitaja kuwa fungu hilo linagharamia makundi makuu matano ambayo ni Kundi la Rais wakiwemo Wasaidizi, Mawaziri au Wakuu wa Taasisi na Walinzi, Kundi la Makamu wa Rais wakiwemo Wasaidizi, Mawaziri au Wakuu wa Taasisi na Walinzi na Kundi la Waziri Mkuu wakiwemo Wasaidizi, Mawaziri au Wakuu wa Taasisi na Walinzi.

Makundi mengine ni Kundi la Wakuu wa Nchi na Serikali kutoka nje ya nchi wanapotembelea Tanzania; na Kundi la Wajumbe Maalum wanaokuja nchini kuleta taarifa muhimu kwa Rais. “Makundi yote haya hugharamiwa na Serikali kupitia Wizara ya Mambo ya Nje ndani ya bajeti ya Idara ya Itifaki kifungu cha Ziara za Viongozi.

“Aidha uandaaji wa bajeti ya Wizara chini ya Idara ya Sera na Mipango unahusisha wadau wengine nje ya Wizara kama vile Kamati ya Bunge ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa na hupitishwa kila mwaka na Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,” ilieleza sehemu ya taarifa hiyo.

Kutokana na ufafanuzi huo, iliwatahadharisha wananchi juu ya watu wanaotoa taarifa za uongo kwa madhumuni ya kujenga chuki dhidi ya Serikali. “Ikumbukwe kuwa ziara za viongozi zinazoratibiwa na Wizara ya Mambo ya Nje zina mafanikio makubwa kwa nchi na Watanzania kwa ujumla,” ilisisitiza.

Aidha, ilisema inaandaa taarifa ndefu ya utekelezaji wa majukumu ya Wizara, changamoto na mafanikio yaliyopatikana ndani ya kipindi cha miaka kumi ya uongozi wa Rais Kikwete ambayo itatolewa kwa umma kwa lengo la kutoa elimu zaidi.


CHANZO: Habari Leo

No comments:

Post a Comment