Advertisement

Advertisement

.

.

Mixer

Mixer

Saturday, 5 September 2015

MASHEHE WALIOKUWA WAMETEKWA NCHINI CONGO WAMESEMA KILICHOWASAIDIA NI KUTAJA WANATOKA TANZANIA

Mashehe sita waliokuwa wametekwa na waasi nchini Jamhuri ya Kidemokrasia Congo (DRC) wamerejea nchini jana, huku wakieleza kuwa kulitaja jina la Tanzania kumewaokoa na kifo kutoka kwa waasi hao.

Kitendo cha mashehe hao kutaja wanatokea Tanzania kimewasaidia kwani kwa mujibu wao, waasi hao walisema hawana shida na Tanzania, lakini Wakongo waliwadanganya hivyo hawawapendi.

Akizungumza baada ya kutua katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere, kiongozi wa mashehe hao, Mohammed Abdallah Khamis alisema, wakiwa njiani kuelekea nchini humo walivamiwa na watu hao wakiwa na silaha za kivita kisha kutekwa na kupelekwa porini.

“Mwanzo hatukuelewa kama ni wanajeshi wa serikali au wanajeshi wa porini, tulipofika nao porini ndiyo wakajitambulisha wao ni askari wa porini na wanahitaji fedha ili watuachie ama watatuua,” alisema Khamis.

Akisimulia jinsi walivyoishi porini alisema, walikuwa wanapata tabu kwani hata chakula walikuwa wakipewa ndizi, maharage na magimbi ambayo waliambiwa wale ili wasife, huku wakati mwingine wakiteswa na waasi hao kwa kupigwa na magongo na vibao.

Alisema waasi hao walihitaji wapewe kiasi cha dola za Marekani 20,000 (zaidi ya Sh milioni 60) ili waweze kuachiwa. 


Aidha, Khamis aliishukuru serikali ya Tanzania kwa jitihada ilizofanya ili kuhakikisha wapatikana wakiwa salama. “Kwa kweli tunaipongeza sana serikali ya Tanzania na DRC maana wamefanya juhudi kubwa sana za kutuokoa.  

Kwa upande wake Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Mahadhi Juma Maalim akizungumza baada ya kuwapokea mashehe hao alisema, wakati wote serikali ilikuwa ikifuatilia suala hilo ili kujua usalama wao, huku akisema kwamba kuna umuhimu kwa Watanzania wanaosafiri kwenda katika nchi tofauti kwa shughuli mbalimbali kuhakikisha wanatoa taarifa katika Balozi zilizopo katika nchi hizo ili serikali iwe na taarifa ya Watanzania hao.

No comments:

Post a Comment