Advertisement

Advertisement

.

.

Mixer

Mixer

Saturday, 26 September 2015

RIPOTI KUHUSU WATANZANIA WALIOKUFA WAKATI WAKISHIRIKI IBADA YA HIJJA

Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, imethibitisha kutokea kwa vifo vya mahujaji Watanzania wanne, waliokufa wakati wakishiriki ibada ya Hijja, iliyofanyika Makka, Saudi Arabia juzi.

Taarifa ya wizara hiyo iliyotumwa kwa vyombo vya habari jana, ilieleza kuwa Ubalozi wa Tanzania nchini Saudi Arabia, umeeleza kuwa mahujaji hao walikufa kutokana na msongamano mkubwa wa watu uliotokea kwenye eneo la Mina.

Miongoni mwa waliokufa na kutambuliwa kwa mujibu wa taarifa hiyo ni Mwanaisha Hassan Juma, Mkungwe Suleiman Hemedi na Sefu Saidi Kitimla, huku taratibu zikiendelea kuchukuliwa kutambua mwili wa Mtanzania wa nne.

“Ubalozi unaendelea na jitihada za kupata jina la Mtanzania mwingine aliyekufa kwenye tukio hilo. Aidha, Serikali ya Saudia imeahidi kutoa taarifa kamili, ikiwemo idadi ya watu waliokufa na majeruhi na nchi wanazotoka mara itakapokamilika,” ilieleza taarifa hiyo.

Mbali na Watanzania hao wanne, taarifa hizo zimeeleza kuwa kuna mwingine aliyetokea nchini Tanzania na kufa katika tukio hilo, Fatuma Mohammed Jama, ambaye imebainika ni raia nchi jirani ya Kenya. “Mtu mwingine aliyekufa ni raia wa Kenya anayeishi nchini, ambaye ametambulika kwa jina la Fatuma Mohammed Jama,” imeeleza taarifa hiyo.

Taarifa hiyo ilieleza kuwa Ubalozi wa Tanzania nchini humo, kwa kushirikiana na taasisi zinazoshughulikia masuala ya Hijja za Tanzania, ikiwemo Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (Bakwata) na mamlaka za Serikali ya Saudi Arabia, wanaendelea kufuatilia kwa karibu ili kujua endapo kuna vifo na majeruhi wengine kutoka Tanzania.

Kutokana na hali hiyo, Serikali imewaomba wananchi kuwa watulivu katika kipindi hiki kigumu wakati Serikali ikiendelea kufuatilia.

Rambirambi za Rais Kikwete Kwa upande wake, Rais Jakaya Kikwete ametuma salamu za rambirambi kwa Mfalme wa Saudi Arabia, Salman bin Abdulaziz Al Saud kutokana na vifo vya zaidi ya mahujaji 700 vilivyotokea juzi.

Chanzo: Habari Leo

No comments:

Post a Comment