Monday, 7 September 2015

TANESCO YATANGAZA NCHI KUINGIA GIZANI KWA WIKI NZIMA

Shirika la umeme nchini (TANESCO), limetangaza nchi kuingia ‘gizani’ kwa wiki nzima kuanzia leo kutokana na kuzimwa kwa mitambo ya gesi inayozalisha umeme kutoka Songosongo na kuanza majaribio ya gesi ya Mtwara.
 

Mkurugenzi Mkuu wa Tanesco, Felchism Mramba, aliwaambia waandishi wa habari jana baada ya kutembelea mtambo wa Kinyerezi I, kuwa sasa Watanzania wategemee umeme wa uhakika baada ya kuanza kuzalisha umeme kwa gesi ya Mtwara.

Alisema tayari gesi imeanza kuingia kwenye mtambo wa Kinyerezi I na Ubungo II na kwamba kinachofanyika sasa ni majaribio ya kusukuma mitambo ya Ubungo II na Symbion kwa ajili ya uzalishaji.

“Kwa hiyo kesho (leo), tutazima mitambo yote ya gesi ya Songosongo ili kuanza kazi ya kuunganisha bomba la gesi kutoka Mtwara…wakishaunga, kutakuwa na kazi ya kufanya majaribio ya hapa na pale, kazi ambayo tunategemea itachukua kama wiki moja hivi,” alisema.

Aidha, aliongeza kuwa: “Wananchi wamekuwa wakifuatilia sana umeme, lakini niwaambie tu kuwa tutaenelea kuwa na tatizo hadi Septemba 15 kwa sababu tunataka kuingiza kitu kipya, lakini tunategemea baada ya wiki moja, umeme utaongezeka zaidi.”

Alisema hali ya umeme kwa siku ya leo itakuwa mbaya zaidi kwa kuwa ‘mitambo yote itakuwa imezimwa.’

Alisema kazi ya kuunganisha bomba hilo itaihakikishia nchi kuwa na umeme wa uhakika hata kama mabwawa ya maji yanayotumiwa kuzalisha umeme yatakuwa yamekauka.

Alisema gesi ya Mtwara inategemewa kuendesha mtambo wa Ubungo II wenye uwezo wa kuzalisha MW 105, Symbion (MW 112) na Kinyerezi I (MW 150).

Mramba alisema mtambo wa Ubungo I utaendelea kuzalisha umeme kwa kutumia gesi ya Songosongo na kwamba Ubungo II inatumia gesi ya Mtwara kwa kuwa inatosha kuendesha mitambo hiyo.

No comments:

Post a Comment