Saturday, 24 October 2015

LEO NI LEO VIGOGO WA CCM KUFUNGA MIKUTANO YA KAMPENI NDANI YA MIKOA 7LEO ndiyo siku ya mwisho ya kampeni za urais, ambapo tayari vyama viwili vikubwa, Chama Cha Mapinduzi (CCM) na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), vimeeleza mipango yao ya ufungaji kampeni.

Juzi Chama Cha Mapinduzi (CCM), kilielezea kuwa leo kitafunga kampeni zake za Uchaguzi Mkuu kwa kishindo kwa kufanya mikutano ya kitaifa katika mikoa saba, itakayoongozwa na vigogo wake wa sasa na wastaafu.

Akizungumza Dar es Salaam, Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) na Kamati ya Kampeni, January Makamba alisema mikutano hiyo ya mikoa saba, itaanza saa sita mchana hadi saa 12, ambapo watatumia teknolojia ya kurusha mikutano yote moja kwa moja na vituo vitano vya televisheni na 67 vya redio.

January alisema mkutano mkubwa utafanyika jijini Mwanza na kuongozwa na Mwenyekiti wa Taifa wa CCM, Rais Jakaya Kikwete, Mgombea wa Urais, Dk John Magufuli na Mgombea Mwenza, Samia Suluhu Hassan .

Mkutano wa pili utafanyika Tanga na kuongozwa na Katibu Mkuu, Abdulrahman Kinana na wa tatu utafanyika mkoani Mbeya, ambao utaongozwa na Mwenyekiti mstaafu wa CCM, Benjamin Mkapa.

Mkoa wa nne utakaohusu ufungaji wa kampeni hiyo ya CCM ni Mtwara utakaoongozwa na Mwenyekiti mstaafu, Ali Hassan Mwinyi na mkutano wa Kigoma utakaoongozwa na Makamu Mwenyekiti Tanzania Bara, Philip Mangula.

Mkutano wa sita utafanyika Moshi mkoani Kilimanjaro na utaongozwa na Katibu Mkuu mstaafu wa CCM, Yusuf Makamba na wa saba utafanyika Musoma mkoani Mara na kuongozwa na Waziri Mkuu mstaafu, Joseph Warioba.

Katika Mkoa wa Dar es Salaam, mbali na ufungaji wa kampeni jana, leo wagombea nafasi ya ubunge katika majimbo yote ya Jiji la Dar es salaam, watafunga kampeni katika maeneo ya majimbo yao kwa namna mahususi.

Akitoa tathmini ya kampeni, January alisema CCM imeridhika na ubora na ukubwa wa kampeni zilizofanywa licha ya kuwapo changamoto za hapa na pale na kuwa Dk Magufuli na Samia wamefanya kazi kubwa na walikuwa wakifanya mikutano kati ya nane hadi 12 kwa siku katika siku 57.

No comments:

Post a Comment