Saturday, 10 October 2015

JE, UNAZIJUA SABABU ZA MAGONJWA AKILI? ZOTE ZIPO HAPA LEO


Siku ya Afya ya Akili Duniani, huadhimisha kila tarehe 10 ya mwezi Oktoba kila mwaka duniani kote, huku lengo la siku hii ikiwa ni kuhamasisha jamii juu ya matatizo mbalimbali ya afya ya akili yanayoikabili jamii hususani kutokuthaminiwa kwa utu wao.

Maadhimisho ya mwaka huu yanaongozwa na kauli mbiu isemayo “Utu katika Afya ya Akili (Dignity in Mental Health). Kaulimbiu hiyo imetolewa na Shirikisho la Afya ya Akili Duniani (World Federation of Mental Health) na inalenga kuhamasisha jamii juu ya matatizo mbalimbali ya afya ya akili.


Kwa mujibu wa taarifa ya Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii imesema kuwa lengo kuu la kauli mbiu ya mwaka huu ni kutoa elimu kwa jamii ili waelewe kuwa wagonjwa wa akili wanaweza kuishi maisha yao na kuthaminiwa utu wao kwa kuzingatia sheria za haki za binadamu (Human Right Orientation Policy and Law). Hivyo basi, Tanzania kama ilivyo nchi zingine duniani kote itaadhimisha siku hii ambapo Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii (WAUJ) kwa kushirikiana na Chama cha Wataalamu wa Afya ya Akili Tanzania (MEHATA) itaadhimisha siku hii kwa kutoa elimu kuhusu umuhimu wa kuzingatia utu wa mgonjwa wa akili pale anapokwenda kupata huduma za matibabu katika vituo vya kutolea huduma.


Wizara pia imeainisha kwamba maelfu ya wagonjwa wa akili Duniani kote wanakosa haki zao kama binadamu, lakini pia wagonjwa wa akili wamekuwa wakitengwa, kubaguliwa na kunyanyapaliwa pamoja na kunyanyaswa kihisia (emotional abuse) pamoja na unyanyasaji wa kimwili (physical abuse) katika jamii.


Taarifa hiyo ya wizara ya afya pia ilifafanua kuhusu afya ya akili na kusema kwamba magonjwa ya akili ni magonjwa ambayo yanaathiri uwezo wa mtu kufikiri, kuhisi, kutambua na kutenda, na hivyo kuwa na tabia au mwenendo uliotofauti au usioendana na jamii husika kiimani, kimila, desturi, na nyanja nyingine za kijamii. Tabia hizo zinatokana na ugonjwa wa akili huathiri ufanisi na shughuli za mtu husika (mgonjwa) au huathiri jamii nzima inayomzunguka endapo mgonjwa huyo hatopatiwa matibabu stahiki na kwa wakati muafaka.


Pia wizara imesema kuwa kwa hapa nchini kwetu wagonjwa wengi wa akili hawafiki katika vituo vya kutolea huduma za afya na badala yake kuishia kwenye tiba za jadi au kutelekezwa na kunyanyapaliwa.

Aidha Wizara imezitaja Takwimu na kuonesha kuwa Tanzania ina idadi ya watu takriban milioni 45 na kutokana na taarifa ya afya ya akili kwa mwaka 2014/15 inaonesha kuwa idadi ya watu 817,532 wanaugua magonjwa mbalimbali ya akili nchini, ambayo ni sawa na karibu asilimia 2 ya watanzania wote.


Pia idadi hiyo ni ongezeko la wagonjwa 367,532 ukilinganisha na takwimu za mwaka 2013/14 walikuwa ni 450,000. Kati ya wagonjwa wote wa akili kwa mwaka 2014/15 wanawake ni 332,000 na wanaume ni 485,532, huku mkoa wa Dar es Salaam ukiongoza kwa kuwa na wagonjwa wengi nchini ukifuatiwa na amkoa wa Dodoma na mkoa wa mwisho ni Lindi na kufafanua kuwa idadi hiyo ya wagonjwa ni wale walioweza kuhudhuria katika vituo vya kutolea huduma ya afya hapa nchini.

Mbali na hayo taarifa ya wizara pia imeeleza sababu ya matatizo ya afya ya akili, ikiwa ni pamoja na sababu za kijamii na kisaikolojia kama vile umasikini uliokithiri, kutengwa na jamii, kuwa tegemezi, upweke na upotevu wa vitu mbalimbali (mfano kufiwa na mtu wa karibu, kupoteza mbali, kupoteza kazi au kupata mlemavu), mafarakano katika jamii pamoja na matatizo ya mahusiano, kukosa huduma muhimu, unyanyapaa , unyanyasaji na ubaguzi wa aina mbalimbali.


Sababu nyingine za kibaiolojia ni pamoja na mtoto kupata shida wakati wa kuzaliwa na kusababisha mgandamizo wa ubongo, uchungu wa muda mrefu na mtoto kukosa hewa ya oksijeni, maradhi kwamama mjamzito ambayo hushambulia mfumo wa fahamu wa mtoto aliye tumboni na pia kama wazazi wana vinasaba vya ugonjwa wa akili mtoto/watoto pia wanaweza kurithi.

No comments:

Post a Comment