Friday, 9 October 2015

MAJONZI MENGINE TENA KWENYE SIASAIkiwa bado watanzania hawajasahau majonzi ya kumpoteza Mwenyekiti wa DP Mchungaji Christopher  Mtikila aliyezikwa jana, leo tena kwenye siasa kuna majonzi mengine ambapo Mgombea mwingine wa Ubunge wa Jimbo la Arusha Mjini kwa Tiketi ya Chama cha ACT-Wazalendo, Estomih Mallah amefariki Dunia baada ya kuugua na kukimbizwa Hospitali.

Taarifa ya kwanza ilisema kuwa Mgombea huyo amefariki katika Hospitali ya KCMC Moshi ambapo alikuwa akipatiwa matibabu… Nimempata Msemaji wa Chama cha ACT-Wazalendo, Khamis Abdallah amenifikishia taarifa nyingine kuhusu Kifo cha Mgombea huyo.

“Tatizo lilianza October 06 2015 wakati anajiandaa kwenda kwenye Mkutano wa Mgombea Urais, alisema anajisikia vibaya kichwa kinamuuma… Hakuweza kupanda Jukwaani, akapelekwa Hospitali ya KCMC baada ya hali kuwa mbaya. Jana saa nane usiku tukatumiwa taarifa ya msiba.”


Aidha kuhusu taratibu za kampeni za chama hicho na mazishi Khamis Abdallah amesema "Chama kimesimamisha kampeni mpaka Jumapili, na tumeagiza Bendera za Chama zipepee nusu mlingoti kwenye Ofisi zote za Chama… Chama kitakaa na Familia kuangalia taratibu za msiba na Mazishi."

Mbali na hayo Khamis Abdallah amesema chama cha ACT-wazalendo kimepata pengo kwenye nafasi ya Mgombea Ubunge Jimbo la Arusha Mjini, huku akiongeza kwamba kuhusu masuala mengine hususani ya kampeni tume ndiyo itakayotoa utaratibu wa kuendelea na Kampeni za Ubunge Jimbo la Arusha Mjini baadaye.

Chanzo: Millard ayo.com

No comments:

Post a Comment