Monday, 26 October 2015

MSHINDI WA KITI CHA URAIS KUTANGAZWA RASMI OKTOBA 29Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) imesema mshindi wa kiti cha urais atatangazwa rasmi siku ya Alhamisi na kesho yake, atakabidhiwa cheti tayari kwa kuanza shughuli zake. 

“Tunatarajia Mungu akijalia, siku ya tarehe 29, saa tatu asubuhi, tutatangaza nani mshindi wa kiti cha rais, na tarehe thelathini tutamkabidhi cheti chake aendelee na shughuli zake,” alisema Mkurugenzi wa Uchaguzi, Kailima Kombwey.

Aidha, tume hiyo imesema haina ‘mbeleko’ ya kumbeba mgombea yeyote, bali itatangaza matokeo kama yatakavyokuwa kwenye masanduku ya kura.

“tume hatuna mbeleko…hatuna mbeleko ya kubeba mtu… Tutatangaza matokeo kama yatakavyokuwa. Koleo tutaita koleo, kisu tutaita kisu.” alisema Kombwey

Mkurugenzi wa Uchaguzi, Kailima Kombwey alisema hayo Dar es Salaam jana wakati akizungumza na waandishi wa habari juu ya masuala mbalimbali yaliyojiri katika uchaguzi mkuu uliofanyika jana. Kailima alisema uchaguzi umekwenda vizuri.

Alieleza kuwa matokeo ya awali, yataanza kutolewa leo  asubuhi na yatakuwa yanatolewa kwa awamu tatu au nne kwa siku kuanzia saa 3 asubuhi hadi saa 12 jioni. 


Kombwey alisisitiza kuwa watatangaza ushindi wa kiti cha udiwani, ubunge na urais kulingana na idadi ya kura zilizoko kwenye masanduku ya kura.

Mbali na hayo, Mkurugenzi huyo wa uchaguzi alipongeza kile alichokiita ukomavu mkubwa wa Watanzania, walioonesha kwenye uchaguzi huu ukafanyika kwa amani. Alisema pamoja na kwamba tume ilijiandaa vyema, pia Watanzania wameonesha ukomavu, kiasi cha uchaguzi kutofautiana na wa mwaka 2005 na 2010 ambao zilishuhudiwa vurugu.

No comments:

Post a Comment