Saturday, 3 October 2015

UMEME UMEENDELEA KUKATIKA MARA KWA MARA NCHINI, ZIMETAJWA HAPA SABABU ZOTE ZA TATIZO HILO

Ishu ya kukatika kwa umeme si jambo geni sana miongoni mwa Watanzania wengi kwani umeme umekua ukikatika na kukaa kwa zaidi ya saa kumi na mbili kwenye maeneo mbalimbali Tanzania ikiwemo jijini Dar es salaam.

Mkurugenzi wa TANESCO Injinia Felichesmi Mramba amezungumza yake kuhusu hali hiyo ya kukatika kwa umeme mara kwa mara.

Kuhusu jiji la Dar es Salaam, Mramba amesema katikati ya jiji kuna mradi wa umeme unaojengwa kwa kushirikiana na serikali ya Finland ya kujenga kituo kipya cha umeme katikati ya jiji kitakachokamilika Novemba 2015 hivyo maeneo ya Ilala, Makumbusho na katikati ya jiji yamekua yakizimiwa umeme sababu ya kazi hiyo inayoendelea.

Kuhusu jijini Arusha, Mramba ameyasema haya "kuna kituo kikubwa cha Njiro kimejengwa upya ambapo mjenzi amemaliza kazi yake ila kinachoendelea ni kuunganisha kituo kipya na laini zinazosambaza umeme Arusha.

Aidha, amesema TANESCO imeanza kuwasha mitambo baada ya gesi kufika Dar es Salaam hatua kwa hatua kadri presha inavyofika kwenye bomba, mtambo wa kwanza uliwashwa September 17, mitambo imekua ikiendelea kufanyiwa kazi na kuwashwa hadi leo.

Mramba amesema ikifika tarehe 9 au 10 October 2015 tatizo la kukatika kwa umeme linaweza kuwa limepungua kwa kiasi kikubwa ila tarehe 20 October tatizo ndio litakua limemalizika kabisa nchi nzima.

Mbali na hayo, Mramba amekanusha kile kilichoandikwa kwenye gazeti kwamba TANESCO haina pesa ndio maana hakuna umeme na kusema huo ni 'UONGO."

Hata hivyo, wananchi wametakiwa kuwa na subira, na kueleza kwamba bomba la gesi lilikua jipya na uwashaji mitambo hauwezi kufanywa yote kwa mara moja au kwa siku moja, ni lazima uende taratibu lasivyo kazi iliyofanyika kwa miaka miwili kuteketea ndani ya wiki moja.

Katika hatua nyingine Mramba amesema mitambo mingine ikiendelea kuwashwa hivi karibuni Dar es salaam haitaathiriwa tena na kukatika kwa umeme ila mikoa ya Arusha, Mwanza, Dodoma na Mbeya itapata mkato kidogo mpaka tarehe 7 October, baada ya tarehe 7 Wananchi wataona mabadiliko wenyewe.

Chanzo: Millard ayo.com

No comments:

Post a Comment