Saturday, 10 October 2015

ZIFAHAMU HIZI DALILI ZA MAGONJWA YA AKILI HAPA

Dunia leo inaadhimisha siku ya afya ya akili, siku yenye dhamira ya kuhamasisha jamii juu ya matatizo mbalimbali ya afya ya akili yanayoikabili jamii hususani kutokuthaminiwa kwa watu wenye matatizo hayo.

Siku hii huadhimishwa kila tarehe 10 ya mwezi Oktoba ya kila mwaka na maadhimisho ya mwaka huu 2015 yanaongozwa na kauli mbiu isemayo “Utu katika Afya ya Akili (Dignity in Mental Health)"

Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii tayari imetoa taarifa kuhusu maadhimisho hayo na moja ya mambo ambayo yameainishwa katika taarifa hiyo ya wizara ni pamoja na dalili zinazoashiria magonjwa ya akili ambazo nami nimeona ni vyema wewe msomaji wa www.dkmandai.com ukazifahamu kupitia hapa kama ifuatavyo:

Miongoni mwa dalili za kihisia ni pamoja na kukosa furaha na kuhuzunika sana, kuwa na furaha sana kupita kiasi, wasiwasi au woga kupita kiasi, kupunguza kuongea au kutokuongea kabisa au kuongea sana kupita kiasi, hasira za haraka haraka hata kufikia kupiga wengine na kuwa na msongo wa mawazo.

Dalili nyingine ni kujitenga na watu na kupenda kukaa mwenyewe muda mwingi au kupenda kuwa na watu sana kuliko kawaida, kutokuwa na ari ya kufanya kazi au kufanya kazi nyingi kwa wakati mmoja bila ya kuzikamilisha, Kutokuonyesha hisia yoyote usoni mwake (mf. furaha au huzuni nk), Kutokujijali usafi na muonekano waka pamoja na kuhisi maisha hayana thamani na kuona bora kufa kuliko kuishi na hatimaye kufikia uamuzi wa kujiua na hata kuua wengine.

Hizo zilikuwa ni dalili za kihisia kuhusu dalili za kimwi;i ni pamoja na mwili kukosa nguvu au kuhisi mwili una nguvu sana kupita kiasi, kukosa usingizi au kulala usingizi sana kupita kiasi, kukosa hamu ya kula au kuwa na hamu sana ya kula, kutokutulia (kuhamanika) au kutulia sehemu moja muda mrefu bila ya kujisogeza pamoja na maumivu sehemu mbalimbali za mwili kama vile kichwa, mabega, mgongo, na viungo mbalimbali ambavyo akienda hospitali vipimo havionyeshi tatizo lolote la kimwili.

Dalili nyingine ni za kiakili ambazo ni pamoja na kukosa umakini wa shughuli zako za kila siku, kusahau kwa haraka au kupoteza kumbukumbu, kukosa uwezo wa kupambanua mambo kwa mitazamo tofauti, kusikia sauti ambazo hazipo na kuona vitu ambavyo havipo, imani ya ajabu ambazo haziendani na mila, imani au desturi za jamii yake ; kama vile yeye ni mtu maarufu, au anaamini kuwa yeye ni nabii au anaamini kupokea taarifa kutoka kwenye redio au mitandao ya simu

Dalili nyingine za kiakili ni kuamini kuwa na nguvu ya ziada kutoka nje ya mwili yake inayomsababishia kutenda au kuwaza mambo anayoyawaza pia anaamini mawazo yake yanapunguzwa au kuongezwa na watu wasiojulikana, vyombo vya habari kama vile Radio na TV kuwa vinazungumzia yeye, au vinaongea mawazo yake yeye, lakini pia mawazo yake hayana mtiririko unaoeleweka.

No comments:

Post a Comment