Thursday, 5 November 2015

MANENO YA KWANZA YA RAIS MAGUFULI MARA BAADA YA KUAPISHWA LEO

Leo Novemba 05, 2015 ndio ilikuwa siku maalum ya kuapishwa kwa Dk. John Pombe Magufuli kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na makamu wake Mama Samia Suluhu tayari kwa kuanza kuwatumikia watanzania kwa kipindi cha miaka mitano.

Dk. Magufuli baada ya kuapishwa alitoa Hotuba yake ya shukrani kwa watu mbalimbali baada ya mchakato wa Uchaguzi Mkuu kukamilika.

Miongoni mwa mambo aliyoyasema katika hotuba yake hiyo ni pamoja na kuanza kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutupitisha salama katika uchaguzi huu mkuu.

Aidha, Dk Magufuli amesema amepokea dhamana ya kuiongoza Tanzani kwa nidhamu kubwa sana na kuahidi kufanya kazi kwa juhudi kubwa ili kutimiza ahadi.

Dk Magufuli pia ametumia nafasi hiyo kuvishukuru vyama pinzani, na kusema kwamba vyama hivyo walikuwa ni washindani na sio wapinzani.

"Nawashukuru pia wenzetu wa vyama vya upinzani, mlikuwa washindani na sio wapinzani, nimejifunza mengi," Alisema Dk Magufuli.

Dk Magufuli aliendelea kusema kwamba uchaguzi umekwisha na kuwataka watanzania wote kuungana kwa pamoja na kuweka pembeni itikadi zote na tofauti za kivyama.

Pamoja na hayo Dk Magufuli ametumia hotuba  hiyo kuwashukuru marais wastaafu wote na kusema hana cha kuwalipa zaidi ya kuhakikisha anatunza heshima yao kwa kufanya kazi nzuri.


No comments:

Post a Comment