Friday, 27 November 2015

MARUFUKU KUCHAPISHA KADI ZA X-MAS NA MWAKA MPYA KWA FEDHA ZA SERIKALI


KATIBU Mkuu Kiongozi, Balozi Ombeni Sefue amepiga marufuku utengenezaji na uchapishaji wa kadi za Sikukuu za Krismasi na Mwaka Mpya kwa gharama za Serikali/ umma kwa mwaka huu.

Kwa mujibu wa taarifa ya Ikulu, Balozi Ombeni Sefue amesema yeyote anayetaka kutengeneza au kuchapisha kadi hizo, afanye hivyo kwa gharama zake mwenyewe. Badala yake, aliagiza fedha zilizopangwa kugharimia utengenezaji na uchapishaji wa kadi hizo, zitumike kupunguza madeni ambayo wizara, idara na taasisi za umma zinadaiwa na wananchi na wazabuni waliotoa huduma na bidhaa kwao.

Pia alisema fedha hizo zinaweza kupelekwa katika matumizi mengine ya kipaumbele. Kumekuwa na utamaduni uliojengeka kwa siku nyingi kwa wizara, idara na taasisi za umma kuchapisha kadi za heri za Krismasi na Mwaka Mpya na kuwatumia wadau mbalimbali, na wakati mwingine zikiambatana na zawadi.

Agizo la Sefue, limetolewa siku moja baada ya Rais Magufuli kusitisha maadhimisho ya Siku ya Ukimwi Kitaifa ambayo yalikuwa yafunguliwe mkoani Singida juzi na kufikia kilele chake Desemba mosi mwaka huu mjini humo.

Badala yake aliagiza fedha zote ambazo zilitengwa na serikali pamoja na wahisani mbalimbali kwa ajili ya maadhimisho hayo zielekezwe kununua dawa kwa ajili ya waathirika wa Ukimwi na vitendanishi.

Akizungumza na Televisheni ya Taifa (TBC), Mwenyekiti Mtendaji wa Tume ya Taifa ya Kudhibiti Ukimwi (TACAIDS), Dk Fatma Mrisho, alisema serikali ilitoa agizo hilo juzi wakati tayari Mkuu wa Mkoa wa Singida, Dk Parseko Kone alishafungua maonesho ya maadhimisho hayo.

Katika maadhimisho ya mwaka huu serikali ilitenga kiasi cha Sh milioni 18 kwa ajili ya maadhimisho hayo huku kila mshiriki katika maonesho hayo akichangia kiasi cha Sh 500,000. Mapema wiki hii, Dk Mrisho aliwaambia waandishi wa habari Dar es Salaam kuwa maadhimisho ya mwaka huu yalikuwa yatanguliwe na maonesho ya wadau yatakayojumuisha huduma mbalimbali zikiwamo za utoaji elimu na burudani.

Alisema huduma nyingine zilizopangwa kutolewa katika maadhimisho hayo ya wiki moja ni upimaji wa hiari wa watu zaidi ya 3,500 wanaoishi na virusi vya Ukimwi na utoaji ushauri nasaha, upimaji wa shingo ya uzazi, sukari, uzito, damu na kupata elimu itakayotolewa kupitia vikundi vya sanaa na burudani.

Maadhimisho ya mwaka huu yanachagizwa na kaulimbiu ya ‘Tanzania bila maambukizi mapya ya VVU, vifo vitokanavyo na Ukimwi na ubaguzi na unyanyapaa inawezekana.’

No comments:

Post a Comment