Wednesday, 25 November 2015

MBUNGE WA CCM AKATAA POSHO ZAKE ZOTE ZA MIAKA MITANO ATAKA ZIELEKEZWE KUSAIDIA JAMII

Mbunge wa Singida Magharibi Elibariki Kingu (katikati) akizungumza na waandishi wa habari ambao hawapo pichani

Bunge la kumi na moja linatarajiwa kuanza vikao vyake Januari 2016, lakini kabla ya kuanza kwake tayari mbuge wa Singida Magharibi Elibariki Kingu amethibitisha kutopokea posho za vikao vya bunge.


Mbunge huyo amesema kuwa amefikia maamuzi hayo ili kujiwekea uhalali wa kuikemea serikali ya chama chake CCM katika matumizi yasiyo ya lazima na kuongeza kuwa hana sababu ya kuchukua pesa za posho kwa sababu analipwa mshahara

"Lazima nianze na mimi kwa kutochukua fedha zozote za posho (sitting allowance) wakati wote wa Bunge kwa miaka mitano" alisema Kingu.

Aidha Kingu amesema tayari amemwandikia Katibu wa Bunge kwamba kwa miaka mitano posho zote ambazo ni sawa na zaidi ya milioni 200 haitapita kwenye mifuko yake  bali itatumika kwa akina mama wanaoteseka mahospitalini, watoto wanaokosa madawati na kuboresha miundombinu.

Pia ameendelea kusema kwamba "kwa dhamira safi tukiamua kubana posho mimi na Wabunge wenzangu tutafika mbali, na ninaomba wabunge wenzangu wanisapoti"

Pamoja na hayo, amesema kuwa yeye si wa kwanza kupinga uchukuaji wa posho kwa kuwa kuna watu tayari walianza kuonyesha pia nia hiyo akiwemo Zitto Kabwe, huku akisema anaamini wabunge wengine nao wataonesha uzalendo.

Akifafanua kuhusu jambo hili la kukataa posho kwa wabunge na faida zitakazo patikana Kingu amesema “kama jambo hili la kukataa posho kwa wabunge litatekelezwa kwa wote ni dhahiri tungefika mbali kwa kuwa fedha hizi zingefanya kazi kubwa… Bunge lina jumla ya wabunge 394, vikao vya Bunge kisheria kwa mwaka ni wastani wa vikao 140 mpaka 180, sasa kila mbunge akilipwa 220,000 kila siku kwa wabunge 394, ukipiga hesabu kwa miaka mitano utaona ni kiasi gani cha pesa kitaokolewa”

No comments:

Post a Comment