Monday, 9 November 2015

RAIS DK MAGUFULI: WATANZANIA NIOMBEENI

Rais Dk John Magufuli (wa pili kushoto) na mke wake Mama Janeth Magufuli (kushoto) wakiwa na waumini wengine wa dini ya Kikristo wakati wa misa iliyofanyika Kanisa la Mt. Petro, Dar es Salaam jana. (Na Mpigapicha Wetu).
Rais Dk John Magufuli (wa pili kutoka kushoto) na mke wake mama Janeth Magufuli (wa kwanza kushoto) wakiwa pamoja na waumini wengine wa dini ya kikristo wakati wa misa iliyofanyika katika kanisa la Mt Petro jijini Dar es Salaam

Rais Dk John Magufuli amewataka Watanzania wa dini zote na viongozi wa dini kutoka madhehebu mbalimbali, kuendelea kumuombea ili atekeleze ahadi alizozitoa pamoja na kuinua maisha ya Watanzania.

Dk Magufuli aliyasema hayo kwenye Ibada ya Mavuno iliyofanyika katika Kanisa Katoliki la Mtakatifu Petro lililopo Oysterbay jijini Dar es Salaam jana, huku akiwashukuru pia wananchi wote waliomuombea na kufanikisha kuchaguliwa kuwa Rais wa Tanzania wa Serikali ya Awamu ya Tano.

Rais wa Tanzania, aliwasili kanisani hapo saa 12.50 asubuhi akiambatana na mkewe, Janet. “Natoa shukurani kwa Watanzania wote wenye imani za kidini tofauti kwa sala zao.

Nawaomba waendelee kuniombea ili niweze kutekeleza ahadi nilizotoa, lakini pia niinue maisha ya Watanzania,” alisema Dk Magufuli alipopewa nafasi ya kuzungumza na kuongeza kuwa anaamini kuwa ana deni kubwa kwa Watanzania hivyo aliahidi kufanya kazi kwa bidii na kuboresha utoaji wa huduma kama njia ya kutimiza wajibu wake kwao.

“Sala zenu ni muhimu sana, zitaniwezesha kufikisha nchi yetu katika hatua nyingine bora zaidi,” alisisitiza. Awali, wakati akimkaribisha kanisani hapo, Mwenyekiti wa Parokia ya Mtakatifu Petro, Dk Adelhelm Meru, alisema kwa kawaida Watanzania na Waafrika kwa ujumla wana utamaduni wa kutoa shukurani pale wanapopata mafanikio.

“Huu ni utamaduni tuliorithi tangu vizazi na vizazi ndio maana nakuomba leo mheshimiwa Rais, uje usalimie katika mkutano huu,” alisema Dk Meru ambaye pia ni Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii. Dk Magufuli ni mmoja wa waumini katika parokia hiyo ya Mtakatifu Petro kama ilivyokuwa kwa Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere.

Ibada hiyo pia ilihudhuriwa na waumini wengi ambao pia ni viongozi kama vile Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), Jaji mstaafu Damian Lubuva, Jaji mstaafu Thomas Mihayo na aliyekuwa Balozi wa Tanzania nchini Italia, Profesa Costa Mahalu.

Chanzo: Habari Leo

No comments:

Post a Comment