Tuesday, 24 November 2015

SIKU YA UHURU NI KAZI TURAIS John Magufuli amewataka Watanzania popote walipo kusherehekea siku ya Uhuru, Desemba 9, 2015, kwa kufanya kazi. 

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Ikulu Dar es Salaam jana, ilisema kwamba maadhimisho ya Uhuru ya mwaka huu 2015 yatatumika kama kichocheo cha kujenga tabia ya kufanya kazi (Uhuru na Kazi) nchini.

“Mheshimiwa Rais ameelekeza Watanzania wote siku hiyo waitumie kwa kufanya kazi mbalimbali kama vile mashambani, maofisini, sokoni, viwandani na usafi wa miji yao katika kutimiza dhana ya Uhuru na Kazi kwa vitendo,” ilisema taarifa hiyo.

Aidha, ilisema kwa kuwa sherehe za Uhuru na Jamhuri huendana na maandalizi mbalimbali ambayo yanatumia fedha, kwa kuzingatia kuwa siku hiyo itaadhimishwa kwa kufanya kazi, fedha zilizokuwa zimetengwa kwa ajili ya sherehe hiyo sasa zitumike kwa shughuli zingine za kijamii, ikiwa ni pamoja na kupambana na maradhi hasa kipindupindu, kununulia dawa za hospitali na vitanda vya hospitali kadri kamati za maandalizi zitakavyoamua.

Pia taarifa hiyo ilisema “Ieleweke kuwa sherehe za Uhuru na Jamhuri ni muhimu katika kuadhimisha kumbukumbu ya uhuru wa nchi yetu. Hivyo, sherehe hizi zitaendelea kuadhimishwa kila mwaka kama kawaida kuanzia mwaka 2016,” ilifafanua. Maamuzi hayo ya rais yamefanyika kwa mujibu wa Sheria ya Sikukuu za Kitaifa (The Public Holidays Act, Cap 35) pamoja na Sheria zingine zinazompa mamlaka Rais kutangaza siku yoyote kuwa sikukuu au mapumziko.

Awali, Katibu Mkuu Kiongozi Balozi Ombeni Sefue aliwaeleza waandishi wa habari kwenye Hospitali ya Taifa ya Muhimbili kuwa Dk Magufuli amebadilisha mwelekeo wa namna ya kusherehekea miaka 54 ya Uhuru, Desemba 9, mwaka huu, kwa kuwataka Watanzania kuhakikisha siku hiyo wanaitumia kwa kufanya usafi ili kudhibiti ugonjwa wa kipindupindu. “Ugonjwa wa kipindupindu ni jambo linalomkera Rais Magufuli.

"Amekuwa akisema hivi kweli tunasherehekea miaka 54 ya Uhuru, lakini bado tunashambuliwa na kipindupindu? Ndio maana ameamua kuchukua hatua kwa kuhakikisha nchi nzima wanafanya usafi katika siku hiyo ya kusherehekea Uhuru,” alisema Balozi Sefue. Alisema ugonjwa huo wa kipindupindu chanzo chake kikubwa ni uchafu, hali inayoonesha kuwa bado Tanzania kuna haja kubwa ya kushughulikia uchafu ili kuondokana na magonjwa ya mlipuko kama kipindupindu.

Pamoja na hayo aliwataka wakuu wa mikoa, wakuu wa wilaya, wakurugenzi wa Halmashauri na makatibu tawala wote nchini, kuanza kujiandaa na kuweka mikakati ya namna ya kufanya usafi huo katika maeneo yao, ikiwa ni pamoja na kuandaa vifaa vya kusafishia mazingira. Hii ni mara ya kwanza kwa sherehe za Uhuru kutosherehekewa kwa gwaride tangu Tanganyika (sasa Tanzania Bara) kupata Uhuru wake Desemba 9, 1961 kutoka kwa wakoloni wa Kiingereza.

Balozi Sefue alisema kwa mujibu wa Dk Magufuli, hataki kusikia baada ya Desemba, kuna mgonjwa wa kipindupindu sehemu na kwamba endapo kutakuwa na mgonjwa anayesumbuliwa na ugonjwa huo, mkoa husika uongozi wake watawajibika na kujieleza. Aliwataka wakurugenzi wa Halmashauri, kuhakikisha kuwa sheria ndogo za halmashauri zinazotungwa na kupitishwa zinatekelezwa ipasavyo ili kudhibiti matatizo kama hayo ya uchafu uliokithiri unaosababisha milipuko ya magonjwa.

Kufuatia taarifa hii inaonesha kuwa huu ni muendelezo wa serikali ya Dk Magufuli kubana matumizi ya serikali yake ikiwa ni pamoja na kuchukua hatua kadhaa zikiwamo kufuta ziara za nje ya nchi isipokuwa kwa vibali maalumu, kufuta mikutano isiyo ya lazima katika hoteli kubwa, kupunguza ukubwa wa Baraza la Mawaziri na sherehe mbalimbali kama ile ya uzinduzi wa Bunge hilo la 11.


No comments:

Post a Comment