Monday, 9 November 2015

VIONGOZI WA DINI WAMEOMBWA KUENDELEA KUIOMBEA ZANZIBAR

Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan 
Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan amewaomba viongozi wa dini kuiombea Zanzibar ili dosari zilizojitokeza wakati wa Uchaguzi Mkuu zipatiwe mwafaka wa kiungwana.

Akizungumza katika ibada maalumu ya kumshukuru Mungu kwa kudumisha amani na utulivu kabla na baada ya uchaguzi iliyofanyika kwenye Ukumbi wa Diamond Jublee, Dar es Salaam jana, Samia alisema kwa hali ya kisiasa iliyopo Zanzibar, ni dua za Watanzania za kumlilia na kumwangukia Mungu zinazotakiwa ili kudumisha amani visiwani humo.

“Maombi yenu hayawezi kupotea bure. Kwa dua zenu dosari ndogo zilizojitokeza huko Zanzibar zitapatiwa mwafaka wa kiungwana hivi karibuni,” alisema Samia katika ibada hiyo iliyoandaliwa na Kamati ya Amani ya Mkoa wa Dar es Salaam kwa kushirikiana na Kanisa la Agape.

Alisema kutokana na uchaguzi wa mwaka huu kukabiliwa na changamoto kadhaa, kuna watu waliamini kuwa Tanzania isingetoka salama. “Naamini bado Mungu anawapenda Watanzania jambo hilo limemalizika kwa salama na amani,” alisema.

Alitoa mwito kwa Watanzania wote kulinda na kudumisha amani na pia akasema jambo hilo lisifanyiwe mzaha na mtu yeyote, kwani amani ikitoweka taifa litapukutika na kutoweka pia.

Alisisitiza kuwa serikali imejipanga kuhakikisha wanasimamia kikamilifu amani na hawatafanya mzaha na mtu yeyote yule ambaye kwa maslahi yake au kikundi kidogo, atadiriki kuvuruga amani ya Watanzania walio wengi.

Pia aliwakumbusha waumini wa dini zote nchini kuendelea kupendana na kuvumiliana kiimani na kwamba tofauti zao za kiimani au kuabudu haziondoi haki yao ya kuwa watoto wa baba mmoja ambaye ni Mungu na kwamba nyumba yao ni moja, yaani Tanzania.

“Hakuna dini bora kuliko zingine. Dini zote ni sawa, tofauti yake ni utaratibu na namna ya kuabudu. Pendaneni kwani dini zetu zote zinatufundisha kuwapenda hata maadui wanaotuudhi,” alisema Samia.

Naye Mwenyekiti wa Kamati ya Amani, Alhad Musa Salum, alisema kabla ya uchaguzi kamati hiyo ilihubiri amani na kuwaomba wananchi wadumishe amani hiyo na jana walikuwa wanamshukuru Mungu kwa kusikiliza maombi yao.

Shekhe Hemed Jalala akizungumza kwenye ibada hiyo alisema Serikali ikiwa karibu zaidi na viongozi wa dini ana hakika nchi itaendelea kubakia kisiwa cha amani na taifa halitambagua Muislamu au Mkristo.

Kiongozi wa Agape, Dk Venon Fernandes alisema wamefanya ibada hiyo kwani sio vizuri kuendelea na biashara baada ya uchaguzi bila kumshukuru Mungu kwa kudumisha amani na utulivu katika nchi yetu.

Alisema kupitia kituo chake cha televisheni kuanzia mwaka jana waliwaomba watu mbalimbali wajitokeze kuliombea taifa hili linapoelekea kwenye uchaguzi mkuu na Mungu amesikia maombi yao. “Inabidi tumshukuru Mungu kwa amani hii, hatuwezi kuendelea na biashara zetu bila kutoa shukrani,” alisema Dk Fernandes.

No comments:

Post a Comment